Kwa nini utawala wa Kizayuni hauna uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya makombora ya muqawama wa Yemen?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130080-kwa_nini_utawala_wa_kizayuni_hauna_uwezo_wa_kukabiliana_na_mashambulizi_ya_makombora_ya_muqawama_wa_yemen
Maafisa wa utawala wa Kizayuni wamekiri kwamba utawala huo hauna uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya makombora ya muqawama wa Yemen, ambayo yanalenga kwa usahihi mkubwa shabaha zilizoko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
(last modified 2025-08-28T02:26:15+00:00 )
Aug 28, 2025 02:26 UTC
  • Kwa nini utawala wa Kizayuni hauna uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya makombora ya muqawama wa Yemen?

Maafisa wa utawala wa Kizayuni wamekiri kwamba utawala huo hauna uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya makombora ya muqawama wa Yemen, ambayo yanalenga kwa usahihi mkubwa shabaha zilizoko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Tovuti ya Kizayuni ya Walla huku ikiashiria katika ripoti yake kwamba Ansarullah ya Yemen hata inachagua kwa umakini mkubwa idadi na maeneo yanayolengwa na makombora hayo, imeandika: "Mahouthi wamefanikiwa kuutwisha utawala wa Israel mfumo wa vita vya kuudhoofisha taratibu kwa kuweka sharti kwamba "maadamu Gaza inashambuliwa, makombora na ndege zisizo na rubani za Yemen zitaendelea kuushambulia utawala huo."

Ripoti hii inasema kuwa, katika kila shambulio linalofanywa dhidi ya Mahouthi huko Yemen, jeshi la Kizayuni hutumai kuwa litakuwa la mwisho na kuwa litafanikiwa kubadilisha mlingano wa nguvu dhidi ya kundi la Houthi, lakini makadirio hayo huwa hayatimii.

Kufuatia operesheni ya makundi ya muqawama ya Palestina ya "Kimbunga cha al-Aqsa" tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi ulianzisha mashambulizi makali na ya kikatili dhidi ya Wapalestina wakazi wa Ukanda wa Gaza. Mashambulio hayo yalikabiliwa na jibu kali la makundi ya muqawama katika eneo, ambapo jeshi na vikosi vya mapambano vya Yemen pia viliingia katika uwanja wa vita kwa lengo la kuyaunga mkono makundi ya muqawama ya Palestina.

Mashambulio ya Muqawama wa Yemen dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu 

Utawala wa Kizayuni kwa kunufaika na uungaji mkono wa Marekani na Magharibi ulizidisha mashambulizi yake dhidi ya miundombinu na miji mbalimbali ya Yemen, ambapo Marekani na Uingereza pia zilishirikiana bega kwa bega na Wazayuni, zikidhani kuwa zingeweza kuwashinda haraka wapiganaji wa Houthi. Lakini kadiri muda ulivyosonga mbele ndivyo vikosi vya muqawama vya Yemen vilivyoishangaza Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni kwa kudhihirisha uwezo na kutekeleza kwa mafanikio makubwa oparesheni zao katika Bahari Nyekundu na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu huko Palestina.

Sababu za kushindwa utawala wa Kizayuni kukabiliana na mashambulizi ya makombora ya muqawama wa Yemen ni mchanganyiko wa udhaifu wa intelijensia, teknolojia na mshtukizo wa kistratijia.

Utawala wa Kizayuni haukutarajia tishio kubwa kutoka kwa Yemen, hivyo droni na mashambulizi ya makombora ya balistiki ya Yemen, hasa makombora ya hypersonic likiwemo la "Palestina 2", yameibua mshtuko na kuchanganyikiwa kukubwa katika mfumo wa makombora wa Iron Dome. Idara za kijasusi za utawala wa Kizayuni pia hazina ufahamu wa kutosha kuhusu muundo, mbinu na maeneo yanayotumika kurushia makombora ya Yemen. Mapungufu haya ya kiintelijensia yamepunguza pakubwa uwezo wa utawala huo wa kuzuia na kukabiliana na makombora hayo.

Mifumo ya makombora ya "Iron Dome" imeshindwa mara kwa mara kuzuia makombora ya Yemen, haswa makombora yenye kasi ya juu ya sauti, ambapo hata baada ya kurushwa hewani makumi ya makombora ya kukabiliana na makombora, hayajafanikiwa kuharibu makombora hayo ya vikosi vya Yemen. Vikosi hivyo vimerusha zaidi ya makombora 200 na ndege zisizo na rubani 170 kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Kiasi hiki cha juu cha mashambulizi kimeweka mfumo wa "Iron Dome" chini ya mashinikizo na hivyo kudhoofisha taratibu uwezo wa kukabiliana nayo.

Yemen inachukulia mashambulizi hayo kama sehemu ya kuunga mkono muqawama wa Wapalestina na kukabiliana na vita vya Gaza. Kiungo hiki cha kistratijia kimeufanya utawala wa Kizayuni ukabiliane na pande kadhaa za vita kwa wakati mmoja. Mashambulio ya anga ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen hayajaweza kuzuia kuendelea kwa mashambulizi hayo ya makombora. Katika ripoti zao, vyombo vya habari vya Kizayuni vinakiri kwamba mashambulizi hayo ya Wazayuni yameshindwa kabisa kistratijia.

Baadhi ya wachambuzi wa vyombo vya habari wenye mfungamano na utawala wa Kizayuni wanakiri kwamba, mashambulizi ya vikosi vya muqawama vya Yemen ni mshtuko wa kiintelijensia na kioperesheni kwa Tel Aviv na kwamba jeshi la utawala huo halina uwezo wa kukabiliana na mrengo huo mpya. Mashambulizi ya hivi karibuni ya makombora ya Yemen katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yameingia katika hatua mpya na ya hali ya juu kabisa, ambayo imetoa changamoto kubwa kwa utawala wa Kizayuni katika masuala ya teknolojia na stratijia.

Mashambulizi ya makombora ya Yemen kwenye maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yameleta mabadiliko katika milinganyo ya kikanda na kijeshi. Mashambulizi haya si ya kushangaza tu katika suala zima la teknolojia na ulengaji sahihi wa shabaha, bali pia yameuweka utawala wa Kizayuni katika hali ngumu kistratijia. Masuala kama utumiaji wa makombora yenye kasi kubwa iliyo juu ya kasi ya sauti, ndege zisizo na rubani zinazojilipua, kulengwa vituo muhimu na mshtukizo wa kistratijia, yote hayo yanaonyesha mabadiliko ya nguvu katika mbinu za mapigano za Yemen na kuongezeka nguvu ya kuzuia hujuma, ya mhimili wa muqawama.

Katika upande wa pili, utawala wa Kizayuni unakabiliwa na changamoto kubwa za udhaifu wa intelijensia, Iron Dome na kushindwa kujibu ipasavyo mashambulio ya adui. Mashambulizi ya vikosi vya Yemen yamethibisha kuwa milinganyo ya nguvu katika eneo hili inabadilika na kwamba pande mpya za mapambano zinaendelea kuundwa, ambazo zinaweza kuwa na nafasi muhimu na taathira kubwa zaidi katika siku zijazo.