Timu ya mazungumzo ya Hamas yawasili Misri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131672-timu_ya_mazungumzo_ya_hamas_yawasili_misri
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza katika taarifa yake ya leo Jumatatu kuwa timu yake ya mazungumzo imeshawasili Misri.
(last modified 2025-10-07T06:01:13+00:00 )
Oct 06, 2025 13:25 UTC
  • Timu ya mazungumzo ya Hamas yawasili Misri

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza katika taarifa yake ya leo Jumatatu kuwa timu yake ya mazungumzo imeshawasili Misri.

Katika taarifa yake hiyo, Hamas imetangaza kuwa, timu ya mazungumzo ya harakati hiyo inayoongozwa na Khalil al-Hayya, mkuu wa harakati ya Hamas katika Ukanda wa Ghaza, imewasili Misri ili kuanza mazungumzo kuhusu utaratibu wa usitishaji vita, kuondolewa vikosi vya Israel vinavyoikalia kwa mabavu maeneo ya Ghaza na kubadilishana mateka.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri kabla ya hapo ilikuwa imethibitisha kwamba awamu ya kwanza na ya kiufundi ya mazungumzo ya kusitisha mapigano Ghaza itaanza Jumatatu huko Sharm el-Sheikh, na kwamba wawakilishi wa Hamas, wa utawala wa Kizayuni na Marekani watakuwepo katika mazungumzo hayo.

Huko Washington, afisa mmoja wa Ikulu ya White House ameiambia televisheni ya Al Jazeera kwamba mjumbe maalumu wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Steve Whittaker, naye alikuweko njiani kuelekea Misri kwa mazungumzo hayo. Afisa huyo aliongeza kuwa mkwe wa Trump na mshauri wake maalumu yaani Jared Kushner, pia atahudhuria mazungumzo hayo.

Kwa upande wake, Hamas ilitangaza katika taarifa yake ya huko nyuma kwamba imekubali kuwaachilia huru mateka wote wa Israel, waliokufa na walio hai kwa masharti kadhaa yakiwemo kuondoka kikamilifu wanajeshi vamzi wa Israel na kufunguliwa mipaka ya kuingizwa huduma muhimu Ghaza. 

Harakati hiyo imesisitiza pia kuwa, mustakbali wa Ukanda wa Ghaza na haki za wananchi wa Palestina zitajadiliwa peke yake na katika nyakati tofauti ndani ya fremu pana ya makundi ya Palestina.