Kiongozi Muadhamu: Umoja wa Wairani umetoa pigo kubwa kwa safu za adui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137936-kiongozi_muadhamu_umoja_wa_wairani_umetoa_pigo_kubwa_kwa_safu_za_adui
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, amepongeza athari kubwa ya umoja wa kitaifa, akisema mshikamano wa wananchi wa Iran umevuruga kwa kiasi kikubwa safu za maadui.
(last modified 2026-04-25T06:12:53+00:00 )
Apr 25, 2026 06:03 UTC
  •  Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei
    Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, amepongeza athari kubwa ya umoja wa kitaifa, akisema mshikamano wa wananchi wa Iran umevuruga kwa kiasi kikubwa safu za maadui.

Kiongozi Muadhamu amesema katika ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Kwa sababu ya umoja wa ajabu uliojitokeza miongoni mwa wananchi wetu, mpasuko umetokea katika upande wa adui.” Amesisitiza kwamba mshikamano huu wa kipekee umevuruga mahesabu ya wale wanaotaka kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Khamenei amesisitiza umuhimu wa kushukuru neema hii ya Mwenyezi Mungu kwa vitendo halisi, akieleza kwamba juhudi kama hizo zitaufanya umoja wa kitaifa uwe “imara zaidi kama chuma,” huku maadui wakibaki “wamedhalilika na kudhoofika zaidi.”

Kiongozi huyo pia ameashiria vita vinavyoendelea vya kisaikolojia vinavyoendeshwa na maadui, akionya: “Operesheni za vyombo vya habari vya adui, kwa kuhujumu fikra za wananchi, zinalenga kudhoofisha umoja na usalama wa taifa.”

Kwa mujibu wa Press TV, ujumbe wa Ayatullah Khamenei unakuja katika wakati muhimu ambapo Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kusimama imara dhidi ya mashinikizo ya pande nyingi, yakiwemo vikwazo, vitisho, na kampeni za propaganda zinazofanywa na Marekani, utawala wa Kizayuni, pamoja na washirika wao wa Magharibi.

Umoja huu, unaotokana na imani ya kina ya wananchi wa Iran na roho ya kimapinduzi, umejidhihirisha mara nyingi kuwa ngao isiyoshindika, ukigeuza kila njama ya uhasama kuwa fursa ya maendeleo makubwa zaidi.