Jihadul Islami: Mpango wa Trump kwa Gaza unalenga kuwapigisha magoti Wapalestina
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina ya Jihadul Islami amesema kuwa, mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani wa eti kusimamisha vita Gaza unaupendelea tu utawala wa Kizayuni, na unalenga kuwafanya Wapalestina wasalimu amri.
"MUqawama umeonyesha utayari wa kujadiliana kwa msingi kwamba, baadhi ya vipengele vinaweza kushughulikiwa vyema, kwanza kabisa ni kifungu cha kubadilishana wafungwa, amesema Ziyad Al-Nakhala akinukuliwa na televisheni ya Yemen ya Al-Masirah.
Al-Nakhala amesema hayo katika taarifa aliyoitoa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa pili ya ya Operesheni Kimbunga cha Al-Aqsa na kuongeza kuwa, "Iwapo adui anasisitiza kufikia katika mazungumzo kile ambacho hangeweza kufanikiwa katika vita, lazima tusimame kidete na tusiache gharama ya juu iliyolipwa kwa damu ya watu wetu ipotee."
"Kipengele cha kubadilishana mateka kinaweza kukamilika katika siku zijazo, na hivyo kuondoa uwezekano wa mambo kuripuka na visingizio vya adui vya kuhalalisha uchokozi wake," amebainisha kiongozi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina.
"Adui na washirika wake lazima wajue kwamba hatuwezi kusalimu amri kwa masharti na matakwa yao hasa baada ya kujitoa muhanga Wapalestina," ameeleza Al-Nakhala na kuongeza kuwa, "Sisi ndio wamiliki halali (wa Palestina) na lazima tupigane kurejesha haki zetu."
Haya yanajiri huku afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina akinukuliwa akisema kuwa, wawakilishi wa makundi kadhaa ya Wapalestina wamejiunga na timu za mazungumzo huko Sharm el-Sheikh Misri, hatua waliyoitaja kuwa yenye lengo la kufanikisha matakwa ya wananchi wa Palestina.
Makundi ya Palestina yanataka kuhitimishwa vita kuondoka kikamilifu wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel huko kama kama vipaumbele vya wananchi wa Palestina.