Harakati ya BDS yalaani undumakuwili wa Human Rights Watch
Kamati ya Kitaifa ya Palestina ya harakati inayopinga dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina BDS imelikosoa vikali shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kwa kutoa ripoti za upendeleo zinazoakisi haki za Wapalestina, ikiwa ni pamoja na haki ya kurejea katika ardhi za mababu zao, na kudogosha ukiukwaji wa haki za Wapalestina wa Gaza unaofanywa na utawala wa Kizayuni.
Katika taarifa, kamati hiyo imelaani "muelekeo mpya wa ubaguzi wa rangi dhidi ya Wapalestina unaofanywa na Human Rights Watch," ikisema shirika hilo la kimataifa linawanyima Wapalestina haki zao za msingi kimfumo.
Imeongeza kuwa, mwenendo wa hivi karibuni wa HRW unaonyesha chuki za wazi dhidi ya Wapalestina huku ikipuuza ukiukwaji wa haki unaoendelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza.
Kamati hiyo imesisitiza kwamba, haki ya wakimbizi wa Palestina ya kurudi katika ardhi zao ni kanuni isiyoweza kufutwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ikisisitiza kwamba Wapalestina katu hawatakata tamaa.
Haya yanaripotiwa huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendelea kumwaga damu za Palestina wa Ukanda wa Gaza kila leo, mkabala wa kimya cha jamii ya kimataifa.
Vikosi vya jeshi la Israel vimewaua shahidi Wapalestina 3, akiwemo kijana wa miaka 16, katika mashambulizi mapya katika eneo la Zaytoun, kusini mashariki mwa jiji la Gaza, na kuashiria uvunjaji mwingine wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Harakati ya Muqawama ya Wapalestina Hamas.
Kabla ya hapo, mashambulizi makubwa ya anga ya Israel katika Ukanda wa Gaza yaliua shahidi Wapalestina 23, siku moja baada ya watu wengine 14 kuuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel katika vitongoji vya Tuffah na Zeytoun katika mji wa Gaza.