Upinzani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i14581-upinzani_wa_mamlaka_ya_ndani_ya_palestina_kwa_muqawama
Maamuzi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina dhidi ya muqawama wa wananchi wa Palestina yangali yanaendelea; na katika fremu hiyo mamlaka hiyo inatekeleza saisa za kuwapokonya silaha raia wa Palestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 04, 2016 03:46 UTC
  • Upinzani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa muqawama

Maamuzi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina dhidi ya muqawama wa wananchi wa Palestina yangali yanaendelea; na katika fremu hiyo mamlaka hiyo inatekeleza saisa za kuwapokonya silaha raia wa Palestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeweka katika ajenda yake ya kazi mpango unaofahamika kama eti "Ukusanyaji wa Silaha Zisizo na Kibali" ambao utekelezaji wake umezua hasira ya wananchi wa Palestina.

Polisi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wamesisitiza kuwa wataendelea kwa jadi kutekeleza mpango huo kwa  kuzipekua nyumba za Wapalestina ili kukusanya silaha zinazomilikiwa na raia na wanachama wa harakati za Palestina. Makundi ya muqawama ya Palestina  yamekuwa yakikosoa ushirikiano wa kiusalama kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala ghasibu wa Kizayuni, kwa sababu wanaamini kuwa ushirikiano huo wa kiusalama ni kikwazo kikuu cha oparesheni za kijeshi dhidi ya Wazayuni. 

 

Polisi wa Palestina wakipambana na raia wa Kipalestina katika mji wa al-Khalil katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan
 

Imeelezwa kuwa wafungwa wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ni mjumuiko wa wanamapambano wa makundi mbalimbali ya muqawama ya Palestina, ambao walitiwa nguvuni na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kabla ya kutekeleza oparesheni dhidi ya Wazayuni. Tukichunguza utendaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo iliasisiwa kufuatia mwenendo wa mapatano ya Mashariki ya Kati na kufuatia kufikiwa makubaliano ya Oslo, tunaweza kufahamu kuwa shughuli za mamlaka hiyo ni kwa ajili tu ya kusogeza mbele siasa za kupenda kujitanua, ukandamizaji na kuzusha migawanyiko za utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.

Mkataba wa Oslo ulisainiwa mwaka 1993 kati ya viongozi wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina  PLO na wale wa utawala wa Kizayuni; na kufuatia mkataba huo mwaka 1994 ikaasisiwa  Serikali ya Ndani ya Palestina ambayo haikuwa na mamlaka ya kimsingi  ya uongozi.

Kwa msingi huo  tunaweza kusema kuwa Serikali ya Ndani ya Palestina ilizaa mchakato wa mapatano na kwa msingi huo mamlaka hiyo haikuwa na wala haijawahi kuwa na uungaji mkono wowote na uhalali miongoni mwa wananchi wa Palestina.

Kuendelea hatua za Mamlaka ya Ndani ya Palestina za kuwatia nguvuni kwa wingi wanaharakati wa Palestina na kuwapokonya silaha wanamuqawama dhidi ya Wazayuni na wakati huo huo kuimarika nafasi yake ya uingiliaji katika uga wa siasa za Palestina; ambapo kivitendo mamlaka hiyo imekuwa ikihesabiwa kuwa kikwazo katika kupatikana umoja wa Wapalestina, kumewatia hasira zaidi wananchi wa Palestina dhidi ya mamlaka hiyo.

Wapalestina wanaamini kuwa iwapo Mamlaka ya Ndani ya Palestina inataka kuwa na nafasi miongoni mwa raia wa Palestina basi inapasa kutazama upya mienendo yake na kuhitimisha siasa zake za ukiritimba na kuingilia  muqawama wa wananchi wa Palestina kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.

Wananachi wa Palestina wanaamini kuwa, njia pekee ya kufikia malengo yao ni kuendeleza muqawama na kusimama kidete mbele ya utawala wa Kizayuni kwa kuzingatia mafanikio  waliyopata wanamuqawama wa Palestina katika miaka ya hivi karibuni na kutoa vipigo vya mara kwa mara kwa utawala huo katika nyuga za kijeshi na kisiasa. Kulazimishwa kuondoka huko Ghaza utawala wa Kizayuni mwaka 2005 na kutoa pigo kwa utawala huo na hivyo kushindwa kutimiza malengo yake katika vita vitatu vilivyoanzishwa na utawala huo huko Ghaza katika miaka ya hivi karibuni, kunadhihirisha kuwa mapambano yameandaa  msingi wa kufikiwa malengo na matarajio ya Wapalestina. Azma ya kweli ya Wapalestina katika kuendeleza Intifadha inayoonyesha kuwa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa utawala wa Kizayuni kwa lengo la kusitisha Intifadha ya wananchi wa Palestina pia, zimeshindwa kuzuia kuendelezwa mapambano ya ukombozi wa Wapalestina dhidi ya Wazayuni maghasibu huko Palestina.

Vijana wa Kipalestina wakiwa katika mapambano ya Intifadha