Hizbullah: Utawala wa Saudia uache kiburi na utazame upya siasa zake
Mrengo wa Harakati ya Hizbullah katika Bunge la Lebanon umetangaza kuwa, utawala wa Saudi Arabia unapaswa kutazama upya siasa zake.
Taarifa ya mrengo wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon imebainisha kwamba, utawala wa Aal Saud unapaswa kuweka kando kiburi, chuki na kupenda makuu na kuangalia upya mahesabu yake na siasa zake kwani mtetemeko mdogo tu utakaotokea ndani ya utawala huo utakuwa na madhara makubwa katika nafasi ya nchi hiyo.
Taarifa hiyo aidha imeeleza kuwa, nafasi haribifu ya utawala wa Saudia mkabala na Lebanon, Syria, Iraq, Misri, Yemen, Bahrain, Iran na katika nchi nyingine imepelekea kutokea migogoro, machafuko, mapigano na vita huku juhudi zote za kutatua migogoro hiyo na kurejesha amani na uthabiti katika Mashariki ya Kati zikigonga mwamba.
Wakati huo huo, Mrengo wa Harakati ya Hizbullah katika Bunge la Lebanon umebainisha kwamba, kuanza tena mazungumzo ya kitaifa nchini Lebabnon ni jambo la dharura na ni kwa manufaa ya nchi hiyo.
Tangu tarehe 25 Mei 2014 baada ya kumalizika kipindi cha urais wa Michel Suleiman, Lebanon imekumbwa na ombwe la kisiasa kwa kubaki bila ya kuwa na rais kutokana na bunge kushindwa hadi sasa kufikia mwafaka juu ya mtu atakayejaza nafasi iliyoachwa wazi na Michel Suleiman. Baadhi ya mirengo nchini Lebanon yenye mfungamano na madolaya Magharibi inatuhumiwa kuwa chanzo cha mkwamo wa kisiasa nchini humo.
Kila mara Wabunge wanapokutana kwa ajili ya kumchagua Rais mpya, kikao hicho hulazimika kuakhirishwa kutokana na kutotimia idadi inayotakiwa kwa ajili ya zoezi hilo la upigaji kura.