Wabunge Iraq wapinga kuweko kijeshi Uturuki huko Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17536-wabunge_iraq_wapinga_kuweko_kijeshi_uturuki_huko_iraq
Wabunge wa Iraq wametaka Uturuki iwekewe vikwazo kama radiamali kwa kuwepo wanajeshi wa nchi hiyo huko Iraq.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 16, 2016 04:36 UTC
  • Wabunge Iraq wapinga kuweko kijeshi Uturuki huko Iraq

Wabunge wa Iraq wametaka Uturuki iwekewe vikwazo kama radiamali kwa kuwepo wanajeshi wa nchi hiyo huko Iraq.

Razaq al Haidari mbunge wa mrengo wa Badr katika bunge la Iraq  amesema kuwa, Uturuki na Saudi Arabia ni chanzo kikuu cha mgawanyiko wa kisiasa huko Iraq na kuitaka serikali ya Baghdad iiwekee Ankara vikwazo vya kiuchumi kutokana na uingiliaji kati wake. Al Haidari amesisitiza kuwa miamala ya Wasaudia kuhusu Iraq inakwenda sambamba na viongozi wa Ankara. Mbunge huyo wa Iraq ameongeza kuwa siasa mbovu za watawala wa Riyadh zimelitumbukiza eneo hilo katika hali ya mchafukoge.

Mbunge mwingine wa Iraq kwa jina la Muafaq al Rubaei ambaye ni Mshauri wa Usalama wa Taifa pia amesema kuhusiana na kuwepo wanajeshi wa Uturuki huko Iraq kwamba mwanajeshi yoyote atakawekuwepo katika oparesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ambaye si wa Iraq, atahesabiwa kuwa ni adui na kukabiliwa vikali. 

Wanajeshi wa Iraq wakijiweka tayari kuukomboa mji wa Mosul

Kwa mara kadhaa sasa Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al Abadi pia ametangaza wazi kuwa anapinga kushiriki wanajeshi wa Uturuki katika oparesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ulioko kaskazini mwa Iraq.