UN: DAESH wamewaua kinyama raia wengi wa mji wa Mosul
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa umepokea ripoti kadhaa zinazoonyesha kuwa, sambamba na vikosi vya jeshi la Iraq kukaribia mji wa Mosul kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeua makumi ya watu wakiwemo maafisa 50 wa polisi ya Iraq ambao wameuliwa kinyama na magaidi wa kundi hilo.
Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, ripoti hiyo ya awali imepokewa kutoka duru za serikali na baadhi ya raia ambao majina yao hayatotangazwa kwa sababu za usalama.
Kwa mujibu wa Coville, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh lilifanya jinai hizo kuanzia siku ya Jumatano hadi Jumapili iliyopita, yaani katika kipindi vikosi vya jeshi la Iraq vilipokuwa vikisonga mbele kuelekea mji wa Mosul ambayo ni ngome ya mwisho ya kundi hilo ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh waliua raia 15 katika kijiji cha Safina kilomita 45 kusini mwa Mosul kisha wakazitupa maiti za watu hao mtoni. Inasemekana kuwa mauaji hayo yalifanywa kwa lengo la kuwatia hofu na kihoro wakaazi wa kijiji hicho.
Siku ya Jumamosi magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh waliwaua kwa kuwapiga risasi wanawake watatu na watoto wadogo watatu wa kike katika kijiji cha Rafila kusini mwa mji wa Mosul.
Rupert Colville amebainisha kuwa maafisa 50 wa polisi ya Iraq waliokuwa wametekwa nyara na kundi la Daesh walinyongwa siku ya Jumapili katika jengo moja kwenye viunga vya mji wa Mosul.
Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za BInadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa: "Tuna hofu kwamba ripoti za matukio ya aina hii hazitokuwa za mwisho kupokea kuhusiana na vitendo vya kinyama vilivyofanywa na kundi la Daesh".
Operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul uliokuwa umevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh tangu mwaka 2014 ilianza tarehe 17 mwezi huu.
Ripoti zinaeleza kuwa hadi sasa vijiji na vitongoji zaidi ya 80 vilivyoko kandokando ya mji huo vimeshakombolewa kutoka kwenye makucha ya kundi hilo la ukufurishaji.../