Mick Napier: Israel inataka kubadilisha demografia ya Ufukwe wa Magharibi, Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21028-mick_napier_israel_inataka_kubadilisha_demografia_ya_ufukwe_wa_magharibi_palestina
Mick Napier, mwanaharakati wa asasi ya Uskochi ya Mshikamano na Palestina amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unaendesha kampeni ya ufutaji kizazi katika Ufukwe wa Magharibi, Bonde la Jordan na maeneo mengine ya Palestina ili kuweza kuanzisha jamii ya "Mayahudi Pekee".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2016 12:53 UTC
  • Mick Napier: Israel inataka kubadilisha demografia ya Ufukwe wa Magharibi, Palestina

Mick Napier, mwanaharakati wa asasi ya Uskochi ya Mshikamano na Palestina amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unaendesha kampeni ya ufutaji kizazi katika Ufukwe wa Magharibi, Bonde la Jordan na maeneo mengine ya Palestina ili kuweza kuanzisha jamii ya "Mayahudi Pekee".

Napier ameiambia kanali ya televisheni ya PressTV kuwa utawala wa Telv Aviv unafanya kila njia kubadilisha mlingano wa idadi ya watu katika Ufukwe wa Magharibi ili idadi ya Wapalestina izidi kupungua na ile ya Mayahudi iongezeke zaidi.

Mwanaharakati huyo wa kutetea haki za Palestina amefafanua kuwa ubomoaji nyumba za Wapalestina unatekelezwa sambamba na mpango mkubwa wa kujenga jamii ya Wayahudi watupu ili kuweza kuanzisha jamii ya kibaguzi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu.

Wapalestina wakibaki bila makaazi baada ya kubomolewwa nyumba yao

Mick Napier amekumbusha kuwa mwaka 1948 Wapalestina walikuwa wakimiliki asilimia 94 ya ardhi ya nchi yao ya Palestina, huku Wazayuni waliokuwa wakitumia "ghilba na nguvu" wakimiliki asilimia 6 tu ya ardhi hiyo; lakini siasa za kujipanua za Wazayuni zimesababisha hali hiyo sasa kuwa kinyume chake.

Zaidi ya Wazayuni nusu milioni wanaishi kwenye vitongoji zaidi ya 230 ambavyo vilianza kujengwa mwaka 1967 sambamba na utawala wa Kizayuni wa Israel kuvamia na kuanza kuyakalia kwa mabavu maeneo ya ardhi za Palestina ya Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas Mashariki.

Askari wa Israel wakibomoa nyumba za Wapalestina

Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa tangu kuanza mwaka huu wa 2016 zaidi ya Wapalestina 1,569 wamebaki bila makaazi kutokana na sera za utawala haramu wa Israel za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.../