Malalamiko ya wananchi wa Yemen kwa Umoja wa Mataifa
Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imeulaumu na kuulalamikia vikali Umoja wa Mataifa na kuutaka utekeleze majukumu yake ya kukabiliana na jinai za ukoo wa Aal Saud nchini humo.
Wizara ya Haki za Binadamu ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imetoa tamko na sambamba na kulalamikia kimya cha Umoja wa Mataifa mbele ya jinai zinazofanywa na Saudi Arabia zikiwemo za kuizingira nchi hyo ardhini, baharini na angani, imekitaka chombo hicho kikubwa zaidi cha kimataifa kutekeleza majukumu yake ya kuwaokoa wananchi madhlumu wa Yemen.
Karibu miezi 20 imepita tangu Saudi Arabia na genge lake waanzishe mashambulizi ya kila upande, ya ardhini, angani na baharini dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen. Hadi hivi sasa vyombo vya kimataifa vinavyojilabu na kujinata kuwa ni viranja wa kupigania haki za binadamu, vinaangalia kwa macho tu namna wananchi wa Yemen wanavyoteketea.
Hata hivyo kwa kuwa nyoyo zimeumbwa na hisia za huruma, walimwengu walio wengi wamekasirishwa na jinai za Saudi Arabia, na wimbi la kulaani jinai hizo linaonekana katika kona mbalimbali za dunia. Pamoja na hayo, Umoja wa Mataifa ambao ulipaswa kuongoza kampeni za kuizuia Saudi Arabia kufanya jinai huko Yemen, kwa mara nyingine umeonesha dhati yake, kuwa ni taasisi dhaifu iliyo tayari kufumba mdomo wake wakati wowote inapotishiwa kunyimwa msaada. Umoja wa Mataifa una historia mbaya ya kushindwa kutatua migogoro duniani licha ya kudaiwa kuwa ni chombo cha kulinda amani na usalama ulimwenguni. Walimwengu hawawezi kusahau namna Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyolegeza misimamo yake kuhusu Saudi Arabia baada ya viongozi wa Riyadh kutishia kusimamisha misaada yao kwa Umoja wa Mataifa. Saudia ilikuwa imewekwa kwenye orodha nyeusi ya wauaji wa watoto wadogo huko Yemen, na tangazo hilo lililotolewa na Katibu Mkuu mwenyewe wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo Ban Ki moon aligeuka kwa digirii 180 na kuitoa Saudia kwenye orodha hiyo baada ya Riyadh kutishia kusimamisha misaada yake kwa chombo hicho cha kimataifa.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kitendo cha Umoja wa Mataifa cha kubadilika ghafla katika misimamo yake kuhusu Saudi Arabia inayofanya mauaji ya umati dhidi ya wanawake na watoto wadogo huko Yemen kwa kushirikiana na mamluki wake, ni ishara mbaya na ya hatari sana. Weledi hao wa mambo wanasema, iwapo taasisi kubwa kama Umoja wa Mataifa uko tayari kufumbia macho mauaji ya kinyama na kubadilisha kikamilifu misimamo yake kwa sababu ya misaada, taasisi nyinginezo za kimataifa zitarajiwe kufanya nini?
Saudia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu na kwa baraka kamili za Marekani, ilianzisha vita vikubwa dhidi ya wananchi wa Yemen mwezi Machi 2015 kwa madai ya kumrejesha madarakani Abdu Rabu Mansour Hadi, rais aliyejiuzulu na kuikimbia Yemen. Saudia inadai kuwa inataka kurejesha utawala wa sheria nchini Yemen, lakini swali linalojitokeza ni kwamba, ni nani aliyeipa Saudia haki hiyo ya kuivamia nchi nyingine bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa na kuanza kufanya mashambulizi ya kiholela?
Kichekesho kingine ni kwamba wakati nchini Yemen kulikuwa kunasikika harufu angalau ndogo ya demokrasia na uhuru wa kiasi fulani wa wananchi kufanya maandamano na kuonesha hisia zao hadharani, wananchi wa Saudia hawasikii hata harufu ya demokrasia na wala uhuru wa kutangaza fikra zao. Swali jengine ambalo viongozi wa Riyadh wanakwepa kulijibu muda wote ni kwamba, ni nani mwenye haki ya kuamua mustakbali wa Yemen, ni wananchi wenyewe wa nchi hiyo au ni madola vamizi yanayoongozwa na Saudia? Je, ukoo wa Aal Saud uko tayari kuruhusu wananchi wa Yemen waivamie ardhi ya Saudi Arabia kwa kila aina ya mashambulizi kwa madai ya kuweka utawala wa sheria na uhuru wa wananchi wa Saudia wa kujichagulia viongozi wanaowapenda?
Kiujumla maswali ya namna hiyo ni mengi na majibu yake yote yanatilia nguvu uhakika usiopingika, wa udhaifu wa kufurutu ada wa Umoja wa Mataifa katika kutatua migogoro ya dunia, udhaifu ambao umeyafanya madola ya kibeberu na vibaraka wao wapate uthubutu wa kuvunja haki ya kujitawala ardhi za nchi nyingine, bila ya woga wowote wa kufuatiliwa kimataifa.