Kukiri duru za Kizayuni juu ya kuwa mbaya hali ya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i22420-kukiri_duru_za_kizayuni_juu_ya_kuwa_mbaya_hali_ya_gaza
Kituo kimoja cha haki za binadamu cha Israel kimekiri kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiifanya kuwa mbaya siku baada ya siku hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2016 04:25 UTC
  • Kukiri duru za Kizayuni juu ya kuwa mbaya hali ya Gaza

Kituo kimoja cha haki za binadamu cha Israel kimekiri kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiifanya kuwa mbaya siku baada ya siku hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Kituo cha Haki za Binadamu cha Israel (Gisha) kimetangaza katika ripoti yake kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiwazuia wagonjwa Wapalestina kutoka katika eneo la Ukanda wa Gaza baada ya kufunga vivuko kwa sababu za kiusalama zisizokubalika. Wagonjwa hao wanahitaji kuondoka huko Gaza ili kwenda kulazwa katika hospitali nje ya eneo hilo kutokana na ukanda huo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa na huduma za kitiba. Israel ilianza kuuwekea mzingiro wa anga, bahari na nchi kavu Ukanda wa Gaza Januari mwaka 2006 baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge.

Lengo la mzingiro huo wa Israel lilikuwa ni kuisambaratisha harakati hiyo ya muqawama. Tangu wakati huo hadi leo, Israel imepuuza matakwa na nasaha zote za kimataifa na kuendeleza mzingiro dhidi ya eneo hilo. 

Maisha ya Gaza

Hatua za kusitasita za jamii ya kimataifa dhidi ya jinai za utawala huo ghasibu hususan inazowafanyia Wapalestina wa Ukanda wa Gaza zimeufanya utawala huo utumie vibaya mazingira ya hivi sasa kwa ajili ya kuzipotosha fikra za waliowengi kuhusiana na uhalisia wa mambo kuhusu Gaza. Hivi sasa Israel inakana kwa kiburi kabisa kuliwekea mzingiro eneo hilo. Katika uwanja huo, idara ya kisiasa na kiusalama ya Wizara ya Vita ya Utawala Haramu wa Israel imedai katika matamshi yake yaliyojaa hadaa kwamba, Gaza haiko katika mzingiro na kwamba, kila siku mamia ya malori yanaingia katika eneo hilo.

Madai hayo yanatolewa katika hali ambayo, duru za Kizayuni zimekiri mara chungu nzima juu ya kuweko mzingiro wa karibu miaka kumi dhidi ya Ukanda wa Gaza uliowekwa na utawala ghasibu wa Israel. Aidha jamii ya kimataifa na maripota wa Umoja wa Mataifa wamekosoa mara nyingi siasa hizo za kidhulma na kutoa wito wa kuhitimishwa mzingiro dhidi ya Gaza. Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanatoa matamshi ya hadaa kwamba, Gaza haiko katika mzingiro katika hali ambayo, kutokana na hofu ya kufichuliwa  mazingira na hali inayotawala huko Gaza, viongozi wa Tel Aviv wamekuwa wakiwazuia maripota wa Umoja wa Mataifa na Majopo ya Kimataifa ya Kutafuta Ukweli kufanya safari katika eneo hilo.

Nyumba za Wapalestima zinavyobomolewa Gaza

Hii ni katika hali ambayo, katika ripoti mbalimbali zinazotolewa na jumuiya na asasi za kimataifa kuhusiana na hali ya mambo katika maeneo ya Wapalestina, kumeashiriwa bayana juu ya athari haribifu na za vifo za kuzingirwa eneo la Gaza na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hivi karibuni Mkutano wa Biashara na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ulitahadharisha katika ripoti yake kwamba, kwa kuzingatia kuwa eneo la Gaza linakabiliwa na mzingiro na limekuwa likiandamwa na mashambulio  ya mara kwa mara ya Israel, yumkini hadi kufikia mwaka 2020 ene hilo likawa halifai kwa ajili ya kuishi.

Hatua za Israel zinaonesha kuwa, licha ya kwamba ililazimika kuondoka Gaza mwaka 2005 kutokana na kushindwa kwake mtawalia na muqawama wa wananchi wa Palestina, lakini ukiwa na lengo la kuonyesha utunishaji misuli, utawala huo umeazimia kufunika kushindwa kwake huko na wakati huo huo kuandaa mazingira ya kuwalazimisha Wapalestina wasalimu amri na  hivyo kuzidi kufanya mauaji zaidi dhidi ya wananchi hao madhulumu.

Madaktari wakimpatia huduma mmoja wa wagonjwa huko Gaza

Kinachotia simanzi zaidi hii leo ni kwamba, kutokana na mashinikiizo ya madola ya Magharibi, jumuiya za kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likitosheka tu na kusikiliza ripoti kuhusiana na jinai za Israel na hakuna hatua yoyote ile linaloichukua ya kusimamisha jinai hizo za Wazayuni maghasibu dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.