Dunia yaendelea kupinga sera za kupenda kujipanua za Israel
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimetoa taarifa tofauti zikilaani hatua ya Israel ya kupasisha ujenzi wa nyumba mpya 2500 za walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Siku nne tu baada ya kuapishwa rasmi Donald Trump kuwa Rais wa Marekani, Waziri wa Vita wa Israel, Avigdor Lieberman na Waziri Mkuu wa utawala huo haramu, Benjamin Netanyahu walipasisha ujenzi wa nyumba mpya 2500 katika Ukingo wa Magharibi.
Baada ya kuchaguliwa Trump kuwa Rais wa Marekani, Israel imezidisha kiburi na sera zake za kupenda kujitanua, na kila leo imekuwa ikipendekeza au kujadili ujenzi wa nyumba mpya na vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina na kupuuza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopiga marufu ujenzi huo. Tunaweza kusema kuwa, misimamo na sera za Marekani za kuiunga mkono Israel kwa hali na mali vimeutia kiburi zaidi utawala huo haramu na kuushajiisha kuendeleza ujenzi wa vitiongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni utawala bandia ulioazishwa katika ardhi ya kughusubiwa ya Palestina kwa kukusanya wahajiri wa Kiyahudi kutoka maeneo mbalimbali duniani na hadi sasa unaendeleza sera za kujitanua kwa kupora ardhi zaidi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi.
Sambamba na hayo inatupasa kusema kuwa, uzembe wa Umoja wa Mataifa na kutochukua kwake hatua madhubuti za kukabiliana na sera hizo za Israel hususan ukiukaji wake wa sheria za kimataifa zinazohusiana na mgogoro wa Palestina, vimeutia kiburi zaidi utawala huo haramu.
Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa zinauzuia utawala ghasibu wa Israel kufanya lolote katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Hata hivyo na kinyume na sheria na maazimio ya kimataifa, Israel imezidisha harakati za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina na kubadili muundo wa kijiografia wa ardhi ya eneo hilo.
Maazimio nambari 242 na 338 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayatambua maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas Mashariki (East Jerusalem) kuwa ni ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na inalazimika kuondoka katika ardhi hizo bila ya masharti yoyote.
Hali ya mambo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina inaonesha kuwa, maazimio yasiyo na maana ya Umoja wa Mataifa ambayo yanalaani kwa maneno matupu sera za kutaka kujitanua za Israel hayawasaidii chochote wananchi wanaopigana kwa ajili ya kukomboa ardhi yao wa Palestina. Katika upande mwingine utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kujitanua na kupora ardhi zaidi za Palestina kwa msaada Marekani, Uingereza na nchi nyingine kadhaa za kimagharibi na kupuuza maazimio ya Barazala Usalama la Umoja wa Mataifa, suala ambalo linazidi kuwadhihirishia walimwengu dhulma na maafa makubwa yanayowapata watu wanaokandamizwa wa Palestina.