PLO yasisitizia kupandishwa kizimbani viongozi wa utawala wa Kizayuni
Katibu Mkuu wa kamati ya utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina ametaka viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wapandishwe kizimbani kwa jinai walizofanya ikiwemo ya ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina.
Saeb Erekat ametoa wito huo mjini Ramallah, Palestina inayokaliwa kwa mabavu katika mazungumzo na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya amani ya Mashariki ya Kati Nikolay Mladenov, na Fernando Gentilini, mjumbe maalumu wa Umoja wa Ulaya katika mchakato wa Amani wa Mashariki ya Kati.
Saeb Erekat amesema wakati sasa umefika kwa maafisa wa Israel kupandishwa kizimbani kutokana na kuendeleza ujenzi wa vitongoji, kwa jinai za vita vya siku 50 vya mwaka 2014 dhidi ya Ukanda wa Gaza na kutokana na kadhia ya Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala huo ghasibu. Afisa huyo mwandamizi wa PLO ameongeza kuwa mafaili ya kesi hiyo yameshawasilishwa na serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Erekat amebainisha kuwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji ni jinai ya kivita, hivyo jamii ya kimataifa ina wajibu wa kulitekeleza azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama linalolaani na kutaka kukomeshwa ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina.
Tarehe 23 Desemba 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kura 14 za 'ndiyo' azimio nambari 2334 linalolaani ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala haramu wa Israel katika maeneo ya Wapalestina.
Kuendeleza ujenzi huo kumeonyesha jinsi utawala wa Kizayuni unavyoendelea kudharau maazimio ya Umoja wa Mataifa, na kuonyesha ulazima uliopo wa kuchukuliwa hatua mpya za kukabiliana na utawala huo ghasibu…/