Fethullah Gülen: Erdoğan ni mnafiki asiyefaa kuaminiwa hata kidogo
Kiongozi wa harakati ya Jama'at Gülen ambaye pia ni mpinzani wa serikali ya Uturuki, amemtumia barua kiongozi wa eneo la Kurdistan nchini Iraq, Masoud Barzani, akimuonya vikali juu ya tabia yake ya kumwamini sana Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki.
Katika barua hiyo ya hivi karibuni Fethullah Gülen, amesema kuwa baadaye Erdoğan, atakuja kumuwinda kwa urahisi Masoud Barzani. Gülen amemuonya juu ya hatma mbaya itakayomkumba kutokana na kuendeleza ushirikiano wake na Rais huyo wa Uturuki sambamba na kufuata siasa zake.
Ameongeza kwa kusema kuwa, kutokana na Masoud Barzani kuwa na mahusiano ya karibu na Rais Recep Tayyip Erdoğan ameingia katika tofauti kubwa na makundi yote ya kisiasa ya kaskazini mwa Iraq kama ambavyo bila ya kuitaarifu serikali kuu ya Baghdad wala makundi ya kisiasa, amesaini mkataba wa kumuuzia Erdoğan na mkwe wake mafuta ya eneo la kaskazini mwa Iraq kwa kipindi cha miaka 50 .
Ameenda mbali kwa kumuonya kiongozi huyo wa eneo la Kurdistan kwamba, bila kuijulisha serikali kuu ya Baghdad, Barzani alimtaka Rais Erdoğan kupeleka majeshi ya nchi yake na kutia kambi katika maeneo ya Mosul, na kusisitiza kuwa, suala hilo limezusha tofauti kubwa baina ya Kurdistan na Baghdad.
Katika sehemu nyingine ya barua hiyo, kiongozi wa harakati ya Jama'at Gülen amemweleza Barzani kwamba, katika kumridhisha Erdoğan, ameamua kutofautiana na Wakurdi wa Syria kwa kubariki jinai za askari wa Uturuki dhidi ya wapiganaji wa kundi la Kikurdi la PKK. Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita, Barzani na Erdoğan walikutana mjini Ankara, Uturuki na baada ya hapo wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga wa nchini Iraq, wakashambulia ngome ya wanachama wa kundi la PKK eneo la Sinjar nchini Iraq. Katika shambulizi hilo la kushtukiza, makumi ya wapiganaji wa PKK waliuawa na wengine kujeruhiwa.
Fethullah Gülen anayeishi Marekani, anasakwa na Uturuki kwa tuhuma za kupanga jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofanyika mwezi Julai mwaka jana nchini humo.