Hizbullah: Iran ni nembo ya izza na uhuru
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29496-hizbullah_iran_ni_nembo_ya_izza_na_uhuru
Naibu Katibu Mkuu wa Hibzullah ya Lebanon amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nembo ya izza na ukombozi duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2017 21:50 UTC
  • Hizbullah: Iran ni nembo ya izza na uhuru

Naibu Katibu Mkuu wa Hibzullah ya Lebanon amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nembo ya izza na ukombozi duniani.

Sheikh Naeem Qassim ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kusisitiza kuwa kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon mwaka 2000 baada ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa muda wa miaka 22 kuliwezekana kwa msaada wa Iran na Syria.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ameeleza kufurahishwa na kufanyika kwa mafanikio uchaguzi wa 12 wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, serikali zote nchini Iran ikiwemo ya Rais Hassan Rouhani zimekuwa siku zote zikiunga mkono Hizbullah na  muqawama.

Katika mahojiano hayo, Sheikh Naeem Qassim ameashiria matamshi ya kifedhuli ya Rais wa Marekani na Mfalme wa Saudi Arabia dhidi ya Hizbullah katika kikao cha Marekani na Waarabu mjini Riyadh na kueleza kwamba, tangu kuasisiwa kwake, Hizbullah imekuwa ikiandamwa kwa njia mbalimbali kwa sababu imesimama kukabiliana na utawala unaoungwa mkono na wakoloni wa dunia, ambao wanafanya kila njia kuuhalalisha na kuufanya ukubaliwe katika eneo utawala huo bandia na mtenda jinai.

Mfalme Salman wa Saudi akimkaribisha Rais Donald Trump wa Marekani

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hizbullah ameeleza pia kwamba, watu wanaotaka harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu ipokonywe silaha wanafanya hivyo kuhudumia maslahi ya utawala wa Kizayuni kwa sababu silaha za Hizbullah hazina nafasi nafasi yoyote ndani ya Lebanon na zinatumika tu kwa ajili ya kupambana na Israel na kudhamini usalama na mamlaka ya kujitawala ya Lebanon.

Sheikh Naeem Qassim amesisitiza pia kuwa Hizbullah itaendelea kuwepo nchini Syria na kufafanua kwamba baada ya kuyakomboa maeneo ya ardhi ya nchi hiyo kutoka mikononi mwa magaidi, Hizbullah haitokuwa na haja tena ya kuendelea kubaki nchini humo kwa sababu inaamini kuwa si jukumu lake kufanya hivyo.../