Mar 13, 2016 06:54 UTC
  • Syria na kukaribia kufanyika mazungumzo ya Geneva

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem amekosoa matamshi yaliyotolewa na Staffan de Mistura, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria na kusisitiza kuwa serikali ya Damascus inaendelea kuheshimu makubaliano ya usitishaji vita.

Al- Muallem aidha ametangaza kuwa ujumbe wa serikali ya Syria utashiriki katika vikao vya mazungumzo ya amani ya Geneva.

Mazungumzo ya amani ya Syria yanatazamiwa kuanza tena hapo kesho mjini Geneva chini ya usimamizi wa mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa nchi hiyo.

Mazungumzo hayo yatahusisha pande mbili za serikali ya Syria na wawakilishi wa makundi ya upinzani.

Mazungumzo hayo yalikuwa yafanyike tarehe 25 ya mwezi uliopita wa Februari, lakini Staffan de Mistura aliyaakhirisha kutokana na hitilafu zilizozuka baina ya makundi ya upinzani.

Nukta muhimu kuhusiana na mazungumzo ya Geneva ni kwamba serikali ya Syria kila mara imekuwa ikitangaza kuwa iko tayari kushiriki mazungumzo hayo; na kuakhirishwa kwake kumetokana na mpasuko mkubwa wa hitilafu za mitazamo uliojitokeza baina ya wapinzani wa serikali hiyo. Serikali ya Damascus imetangaza kuwa kufanya mazungumzo na vikundi vidogo vidogo hakuna tija yoyote; bali inapasa mazungumzo yahusishe kundi kubwa kabisa linaloipinga serikali hiyo ili matunda ya maana yaweze kupatikana kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo. Mtazamo huo unaonyesha kuwa, kuliko ulivyo mrengo wowote wa ndani au nje ya nchi, serikali ya Damascus ina nia ya dhati ya kuhitimisha mgogoro huo wa miaka mitano ambao umesababisha mamia ya maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa, mamilioni kuwa wakimbizi na sehemu kubwa ya miundomsingi ya Syria kuangamizwa.

Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kufanyika mazungumzo ya Geneva, mnamo siku ya Ijumaa

Staffan de Mistura, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria alizungumzia kufanyika uchaguzi wa rais na bunge na kutangaza kuwa chaguzi hizo zitafanyika katika kipindi cha miezi 18 ijayo.

Matamshi hayo ya de Mistura yalikabiliwa na radiamali na jibu kali la Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ambaye alisema mjumbe huyo wa UN hana haki ya kupendekeza ratiba kuhusu jinsi ya kufanyika mazungumzo wala tarehe ya kufanyika uchaguzi; na kwamba hiyo ni haki ya wananchi wa Syria pekee kuamua kuhusu tarehe ya kufanyika uchaguzi.

Mazungumzo ya Geneva kuhusiana na Syria yanaanza hapo kesho katika hali ambayo kwa uapnde mmoja Marekani imetangaza kuwa utatuzi wa mgogoro wa Syria unahitajia njia za kisiasa, si za kijeshi. Na kwa upande mwengine kama ilivyokuwa katika duru iliyopita, hivi sasa pia kungali kuna mpasuko mkubwa wa hitilafu za mitazamo baina ya makundi ya upinzani, huku baadhi ya nchi zilizojihusisha na mgogoro wa Syria kama Saudia na Uturuki zikionyesha kuwa hazijawa na utayarifu kisaikojia wa kuyakubali mazungumzo hayo.

Kutokana na hali hiyo inapasa tuseme kwamba japokuwa katika miezi ya karibuni zimeshuhudiwa waziwazi ishara chanya za kuwa na hamu ya kupoza moto wa mgogoro wa Syria hususan kutoka upande wa serikali za Russia, Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na serikali ya Syria, lakini pamoja na yote hayo inavyoonekana mazungumzo yajayo hayatokuwa na mafanikio zaidi kuliko ya duru iliyopita. Pamoja na hayo, kupatikana tu fursa na mazingira ya kuwezesha kufanyika mazungumzo baina ya makundi ya upinzani na serikali ya Syria ni hatua moja mbele kuelekea kwenye utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo.../

Tags