UN: Nchi zinazohusika ziache kuzipatia silaha pande zinazopigana nchini Sudan
Umoja wa Mataifa umesema, kuendelea kuwasambazia silaha askari wa jeshi na wa vikosi vya wanamgambo wanaopigana nchini Sudan ndiko "kunakowezesha kufanyika uchinjaji" na lazima kukomeshwe wakati raia wa nchi hiyo wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa vita.
"Ili kuweka wazi zaidi, baadhi ya wanaodaiwa kuwa waitifaki wa pande zinazopigana, wanawezesha kufanyika mauaji nchini Sudan", ameeleza Bi DiCarlo alipohutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pasi na kutaja jina la nchi yoyote au pande zozote alizozituhumu kuhusika na uingizaji silaha nchini humo; na akaongezea kwa kusema: "hili si sahihi. Ni kinyume cha sheria, na lazima likomeshwe.”
Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Aprili 15, 2023, kutokana na mzozo wa kuwania madaraka kati ya RSF inayoongozwa na Mohamed Hamdan "Hemedti" Dagalo na mkuu wa SAF Abdel Fattah al-Burhan.
Umoja wa Mataifa unasema vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 24,000 na kusababisha hali mbaya ya maafa ya kibinadamu ambayo imepelekea watu milioni 11 kuwa wakimbizi. Kati yao, karibu watu milioni tatu wamekimbilia nchi jirani, katika janga baya zaidi la watu kuhama makazi yao.
Serikali ya Sudan imeutuhumu Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa unaipatia silaha RSF, tuhuma ambazo zinakanushwa na nchi hiyo. RSF imeripotiwa pia kuwa inapokea msaada wa silaha kutoka kwa kundi la mamluki la Wagner la Russia.../