May 30, 2017 07:47 UTC
  • Ghadhabu ya Wapalestina kufuatia uchozezi wa Israel katika Quds Tukufu

Wapalestina wameendelea kuonyesha ghadhabu zao kufuatia kitendo cha kichochezi cha utawala haramu wa Israel katika mji wa Quds Tukufu unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ametoa taarifa kufuatia kufanyika mkutano wa Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel chini ya  ukuta wa magharibi wa msikiti wa al-Aqsa, ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na ambao Waislamu wanauita kwa jina ukuta wa  Buraq. Hamas imesema hatua ya Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ya kuitisha kikao cha mawaziri wake siku ya Jumapili katika eneo hilo la Quds Tukufu ni matokeo ya safari ya Rais Donald Trump wa Marekani katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu. Nayo Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO imetaja kitendo hicho cha Netanyahu na mawaziri wake kuwa kinyume cha sheria.

Kushadidi vitendo vya kujitanua utawala huo wa Kizayuni kunajiri siku chache tu baada ya safari ya Donald Trump katika ardhi hizo zilizokaliwa kwa mabavu.

Katika safari yake katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, na ambazo zimepewa jina bandia la Israel, Trump alitangaza uungaji mkono wake kamili kwa utawala wa Kizayuni.

Kikao cha kichochezi cha baraza la mawaziri la Israel katika eneo la Msikiti wa Al Aqsa

Kwa msingi huo kufanyika kikao cha baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni chini ya ukuta wa Buraq ni hatua hatari, ya kichochezi na thibitisho kuwa utawala huo wa Kizayuni unalenga kuuyahudisha mji mzima wa Quds (Jerusalem) na kuuhujumu Msikiti wa Al Aqsa.

Safari ya Trump katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina inaonyesha wazi kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel una nafasi ya kipekee katika sera za kigeni za Marekani.

Maingiliano ya kidiplomasia baina ya Marekani na Utawala wa Kizayuni yameongezeka katika kipindi hiki cha utawala wa Trump. Hivi sasa kuna ushirikiano wa karibu baina ya Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa lengo la kuendeleza sera za kujitanua za utawala huo. Hayo yanaendelea sambamba na kutimizwa matakwa ya Marekani katika eneo na wakati huo huo kukanyagwa kikamilifu haki za Wapalestina.

Ushirikiano wa Karibu wa Trump na Netanyahu katika safari ya Trump huko katika  ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu sambamba na hatua yake ya kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu katika safari hiyo kunaonyesha wazi kuwa, Trump atatekeleza kila ambacho Netanyahu anakitaka. Ni kwa sababu hii ndio tunashuhudia Marekani ikishiriki kikamilifu katika sera za kichochezi za Israel za kujitanua zaidi.

Uungaji mkono wa Marekani umepelekea wakuu wa utawala wa Kizayuni wawe na kiburi zaidi katika kushadidisha sera zao za kupora ardhi zaidi na kuwakandamiza Wapalestina.

Netanyahu ameunda Baraza la Mawaziri lenye misimamo mikali zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Baraza hilo limechkua hatua hatari zaidi katika kuendeleza sera za kujitanua za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Wapalestina hasa Quds Tukufu. Utawala wa Kizayuni unazidisha njama zake za kuuharibu Msikiti wa Al Aqsa na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina na hilo limeshadidishwa na baraza la mawaziri wenye misimamo mikali na ya kufurutu ada.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia vibaya migogoro iliyopo katika eneo la Asia Magharibi kwa ajili ya kufikia lengo lake la kuuyahudisha mji wa Quds Tukufu.

Kuongezeka hujuma za walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa Al Aqsa  na pia jitihada za baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni za kueneza satwa yake Quds Tukufu ni mambo yanayoashiria kuwa mji huo ni mhimili mpya wa uchochezi wa Israel katika maeneo mbali mbali ya Palestina.

Katika fremu hiyo ya uchochezi, hatua ya Netanyahu ya kuunda wizara ya masuala ya Quds ni jambo linaloonyesha kina cha njama za Wazayuni dhidi ya mji mtakatifu wa Quds au kwa jina jingine Baitul Maqdis.

Wanajeshi wa Israel wakiuhujumu Msikiti wa Al Aqsa

Hivi sasa wakuu wa utawala wa Kizayuni wanataka kuhamishia huko idara zote za serikali kutoka Tel Aviv. Sisitizo la wakuu wa utawala wa Kizayuni kuhusu madai yao kuwa, Baitul Maqdis ni sehemu isiyotenganika na ardhi zilizotekwa na utawala huo ni utangulizi wa kisiasa wa njama za utawala huo dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa. Mfano wa hilo ni kufanyika kikao cha Baraza la Mawaziri la utawala huo katika eneo la Msikiti wa Al Aqsa.

Wakuu wa Marekani waunaunga mkono mkondo uliochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na wameupa idhini utawala huo kuendeleza sera zake za kujitanua Baitul Maqdis na wana nafasi muhimu katika kusimamia na kuongoza njama hizo za kujitanua Israel huko Quds Tukufu.

Tags