UN: Kipindupindu kimeua watu 600 nchini Yemen Aprili
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29964-un_kipindupindu_kimeua_watu_600_nchini_yemen_aprili
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu umeua karibu watu 600 nchini Yemen ndani ya mwezi wa Aprili pekee mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 02, 2017 22:53 UTC
  • UN: Kipindupindu kimeua watu 600 nchini Yemen Aprili

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu umeua karibu watu 600 nchini Yemen ndani ya mwezi wa Aprili pekee mwaka huu.

Geert Cappelaere, Mkurugenzi wa kieneo wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF amesema katika kipindi hicho cha mwezi mmoja, mbali na kipindupindu kuua Wayemen 600, kesi zaidi ya 70,000 za ugonjwa huo ziliripotiwa pia.

Ameeleza masikitiko yake namna ugonjwa huo unavyoua idadi kubwa ya watu hususan watoto kila siku licha ya kuwa unaweza kuepukika au kutibiwa. 

Afisa huyo wa UNICEF amesema iwapo hali haitadhibitiwa, kesi zaidi ya 130,000 za mripuko wa kipindupindu zitaripotiwa katika nchi hiyo ya Kiarabu ndani ya wiki mbili zijazo.

Watoto ndio wahanga wakuu wa mripuko wa kipindupindu Yemen

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei, Stephen O'Brien, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura aliliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa, Yemen inakaribia kusambaratika kikamilifu huku ikiendelea kukabiliwa na uvamizi wa umwagaji damu ulioanzishwa na Saudi Arabia na kukumbwa na baa la njaa na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu, huku dunia ikiwa inatazama tu.

Kuendelea mashambulizi ya anga ya Saudia na waitifaki wake katika miundombinu, mahospitali, shule na makazi ya raia na kadhalika mzingiro wa kila upande wa nchi hiyo vamizi dhidi ya Yemen, kumepelekea kuenea kwa kasi maradhi kama kipindupindu na magonjwa mengine yanayoteketeza maisha ya wananchi wa Yemen hususan watoto.