Mar 18, 2016 03:09 UTC
  • John Kerry: Ni kweli Daesh wanafuata mafundisho yaliyo kinyume na Uislamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa, ni jambo lisilo na shaka kuwa, kundi la kigaidi la Daesh limetenda jinai kubwa dhidi ya binaadamu.

John Kerry ameyasema hayo mjini Washington mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, wafuasi wa kundi hilo wanafuata mafundisho yaliyo mbali na dini ya Uislamu. Waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Marekani amesema kuwa, kundi la Daesh (ISIS) linawaita Waislamu wengine wa Kisuni na Kishia kuwa ni makafiri na kisha linafanya mauaji ya kutisha dhidi yao. Hata hivyo Kerry amedai kuwa, eti Marekani inafanya juhudi kubwa za kuliwekea ukomo na kulishinda kundi hilo. Amesema kuwa, kundi la Daesh limewaua kinyama raia wasio na hatia wakiwamo Maizadi, Mashia, Masuni na Wakristo. Ameongeza pia kuwa, Daesh wametenda jinai dhidi ya binaadamu na kufanya mauaji ya umati katika maeneo tofauti yanayodhibitiwa na genge hilo. Kerry ametoa matamshi hayo katika hali ambayo ni nchi yake kwa kushirikiana na madola tofauti ya duniani ukiwemo utawala haramu wa Kizayuni, Saudia, Qatar, Uturuki nk, ndio waungaji mkono wakubwa wa kifedha na kisilaha kwa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri.

Tags