Sep 19, 2022 10:59 UTC
  • John Kerry wa Marekani akosolewa kwa kupuuza mabadiliko ya tabianchi Afrika

Wanaharakati wa hali ya hewa safi kutoka nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara, wamemkosoa vikali mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya tabianchi John Kerry kwa kutoa ahadi za uongo kuhusu kusaidiwa bara la Afrika kukabiliana na athari mbaya za uchafuzi wa hewa.

Wanaharakati hao wamesema Kerry, ambaye alihutubia kikao cha 18 cha Mkutano wa Mawaziri wa Afrika kuhusu Mazingira (AMCEN) uliofanyika Septemba 13 hadi 16 huko Dakar, Senegal, alionekana kutojali matatizo ya watu wanaoishi katika mazingira magumu katika bara hilo linalobeba mzigo mkubwa wa msukosuko wa hali ya hewa pamoja na kuwa linachangia sehemu ndogo sana ya uchafuzi huo.

Mithika Mwenda, mkurugenzi mtendaji wa Muungano wa Uadilifu na Haki katika Mabadiliko ya Tabianchi Afrika (PACJA) wenye makao yake Nairobi, amekosoa hotuba ya Kerry na kusema kwamba ilikuwa na mapungufu ambapo Marekani na Magharibi hazijtekeleza majukumu yao kuhusu  azma ya Afrika ya kutumia nishati kijani.

Kwa mujibu wa Mwenda, mataifa makubwa ya Magharibi bado hayajatimiza ahadi zao za kusaidia Afŕika kukabiliana na msukosuko wa mabadiliko ya tabianchi unaozidi kuongezeka ambao umezidisha umaskini, kukosekana usawa, migogoro na milipuko ya magonjwa.

Uchafuzi wa mazingira katika nchi tajiri kiviwanda ni moja ya sababu za ukame Afrika

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Afrika huchangia asilimia 2-3 ya uchafuzi wa mazingira ya dunia lakini bara hilo limeathirika zaidi na uchafuzi wa mazingira katika nchi tajiri kiviwanda.

Kati ya athari za uchafuzi wa mazingira duniani ni ukame, mafuriko na kuongezeka maji baharini mambo ambayo yamezisababishia nchi za Afrika matatizo makubwa. Kwa msingi huo nchi za Mahgairbi zinapaswa kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na athari mbaya za uchaguzi wa mazingira lakini hazifanyi hivyo.

Tags