Duru za Kizayuni zakiri kuwa Israel inayaunga mkono makundi ya kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33890-duru_za_kizayuni_zakiri_kuwa_israel_inayaunga_mkono_makundi_ya_kigaidi
Utawala wa Kizayuni umekiri rasmi kuwa unawapatia misaada makundi yanayobeba silaha huko Syria na yale ya kigaidi yanayopigana dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Uungaji mkono wa utawala huo kwa makundi hayo yanayobeba silaha ni wazi kuwa hauishii tu katika kuwapatia matibabu wanamgambo majeruhi katika hospitali za Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 03, 2017 02:28 UTC
  • Duru za Kizayuni zakiri kuwa Israel inayaunga mkono makundi ya kigaidi

Utawala wa Kizayuni umekiri rasmi kuwa unawapatia misaada makundi yanayobeba silaha huko Syria na yale ya kigaidi yanayopigana dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Uungaji mkono wa utawala huo kwa makundi hayo yanayobeba silaha ni wazi kuwa hauishii tu katika kuwapatia matibabu wanamgambo majeruhi katika hospitali za Israel.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limewanukuu viongozi wa ngazi za juu wa Israel na kuandika kuwa uungaji mkono wa kijeshi wa jeshi la Israel kwa mamluki wenye silaha huko Syria mwaka huu unakadiriwa kuwa wa zaidi ya shekel milioni 115 fedha za Israel ambazo ni sawa na dola zaidi ya milioni 32. Ripoti hiyo imefafanua kuwa kiwango hicho cha pesa hakijumuishi gharama za matibabu za mamluki wenye silaha wanaojeruhiwa huko Syria ambacho kinakadiriwa kuwa ni makumi ya mamilioni ya shekel; na gharama zote hizo hulipwa na Wizara za Usalama, Fedha na Afya za Israel. Jeshi la Israel huko nyuma liliwahi kukiri kuwa idadi ya wanamgambo mamluki waliojeruhiwa huko Syria ambao hivi sasa wanatibiwa katika hospitali za Israel wamefikia 1400; idadi ambayo inazidi kuongezeka katika hospitali za Israel  huku gharama za kila siku za kulazwa kwenye hospitali hizo zikiwa ni shekel 2500 sawa na karibu dola 750. 

Mahusiano hayo makubwa kati ya Israel na magaidi yamefichuliwa katika hali ambayo katika mazungumzo kati yake na Rais Vladimir Putin wa Russia hivi  karibuni, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alitoa madai ya dhihaka na kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaliunga mkono kundi la Daesh bila ya kuashiria mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya jeshi la Syria katika kuwaunga mkono magaidi wa Daesh na wa kundi la Jabhatul Nusra. 

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni  

Hii ni katika hali ambayo Moscow mara kadhaa imekadhibisha madai hayo ya utawala wa Kizayuni na kutangaza kuwa Russia, Iran na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ziko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugaidi. Utawala wa Kizayuni kwa kutoa tuhuma hizo zisizo na msingi, una lengo la kuzipotosha fikra za waliowengi kuhusu uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya utawala huo na magaidi hao wa kitakfiri.  

Ni wazi kuwa makundi ya kigaidi yaliyopo katika nchi za eneo hili khususan huko Iraq na Syria yasingeweza kufika hapo yalipo bila ya kuungwa mkono kifedha na kisilaha na baadhi ya pande ajinabi ukiwemo utawala wa Kizayuni na hivyo kuyawezesha kutenda jinai na kuzusha migogoro chungu nzima. Kuongezeka harakati za kijeshi za utawala wa Kizayuni dhidi ya Syria sambamba na  fitina za utawala huo za  kuishughulisha Syria na migogoro ya ndani hakubakishi shaka yoyote kwamba wimbi linalofanywa na ugaidi wa kuagizwa kutoka nje dhidi ya nchi za Mashariki ya Kati khususan Syria zimetokana na njama hatari za utawala wa Kizayuni, madola ya Magharibi na vibaraka wao.  

Katika mazingira kama hayo utawala wa Kizayuni umeazimia kushadidisha mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Syria kukiwemo kuyashambulia maeneo ya karibu na mji mkuu wa Syria ili kuandaa fursa ya kuendelezwa hujuma za magaidi katika vituo vya  kistratejia vya Syria na hivyo kuwaandalia magaidi upenyo wa kuendelea kuwepo huko Syria.  

Ni katika fremu hiyo ndipo waungaji mkono wa magaidi ikiwemo Marekani, serikali za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wakawa wanahangaika huku na kule ili kufikia lengo hilo. Katika hali kama hiyo misaada inayotolewa na utawala wa Kizayuni kwa makundi yenye silaha ya kitakfiri huko Syria imeingia katika awamu mpya kwa kuasisiwa makundi ya mawasiliano. Kuhusiana na suala hilo Ohad Hamo Mtaalamu wa Masuala ya Kiarabu wa Kanali ya 2 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni amekiri kuhusu makundi hayo ya mawasiliano kati ya Israel na magaidi huko Syria na kueleza kuwa: Idara za siri za intelijinsia zinaasisiwa kwa lengo la kuwafikishia misaada magaidi wa kitakfiri huko Syria. 

Magaidi wa kitakfiri wa kundi la Daesh (ISIS)

 Ghalib Qandil Mwandishi na Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa pia amesema kuwa: Utawala wa Kizayuni kwa kuyaunga mkono makundi ya kitakfiri yenye silaha huko Syria una lengo la kuingia katika ardhi ya nchi hiyo. Qandil ameongeza kuwa  utawala wa Kizayuni umeasisi makundi ya mawasiliano baina yake na makundi ya kigaidi huko Syria ili kunufaika zaidi na taarifa za kiitelijinsia na kiusalama za Syria.  

Matukio ya Syria yanaonyesha kuwa mgogoro wa nchi hiyo kimsingi umesababishwa na uingiliaji wa kigeni, misaada ya kifedha na silaha inayotolewa kwa magaidi sambamba na kuendelea kuingia huko Syria magaidi ambapo Marekani na Israel zimekuwa na nafasi kuu takribani katika masuala yote hayo.