Matukio ya kisiasa na kiusalama ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3616-matukio_ya_kisiasa_na_kiusalama_ya_yemen
Muhammad Abdus Salam, msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, wamefikia maafikiano na Saudia kuhusu kuanza hatua za kujenga hali kuaminiana kwa shabaha ya kukomesha kikamilifu vita na mapigano nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 22, 2016 23:14 UTC
  • Matukio ya kisiasa na kiusalama ya Yemen

Muhammad Abdus Salam, msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, wamefikia maafikiano na Saudia kuhusu kuanza hatua za kujenga hali kuaminiana kwa shabaha ya kukomesha kikamilifu vita na mapigano nchini Yemen.

Muhammad Abdus Salam alisema hayo Jumatatu wakati alipohojiwa na televisheni ya al Mayadeen na kuthibitisha habari zinazosema kuwa, harakati ya Ansarullah imefanya mazungumzo ya moja kwa moja na Saudia. Amesema, kuna maafikiano ya aina fulani yamefikiwa baina ya pande hizo mbili kuhusu kuanza hatua za awali za kujenga hali ya kuaminiana kwa shabaha ya kusimamisha kikamiliifu vita na mashambulizi huko Yemen. Ameongeza kuwa, katika hatua ya kwanza ya mazungumzo, pande mbili za Ansarullah na Saudia zilibadilishana mateka kama hatua ya awali ya kujenga hali ya kuaminiana na kwamba katika hatua hiyo ya kwanza, Saudia iliwaachilia huru wanamapambano saba wa Yemen katika mkabala wa kuachiliwa huru mwanajeshi wake mmoja. Msemaji wa Ansarullah ameongeza kuwa, hadi hivi sasa karibu maiti 70 za pande hizo mbili zimeondolewa kwenye mistari ya mbele ya mapigano na juhudi zinafanyika kuondoa maiti zaidi. Vile vile amesema, pande hizo mbili zimekubaliana pia kusimamisha vita katika mistari ya mbele ya mapigano na jambo hilo linatarajiwa kuishia kwenye kusimamishwa vita kikamilifu nchini Yemen haraka iwezekanavyo. Shirika la habari la DPA la Ujerumani limeripoti kuwa, makundi yote hasimu nchini Yemen na Saudia yanasisitizia haja ya kusimamishwa vita na kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Ismail Ould Sheikh Ahmad, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amesema kuwa, pande zote hasimu katika mgogoro wa Yemen zimekubaliana kusimamisha vita na kuanza mchakato wa kisiasa wa kukomesha mgogoro wa nchi hiyo pamoja na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa huko Yemen. Wakati huo huo Hussein Amir Abdollahiyan, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika amezungumza kwa njia ya simu na Ismail Ould Sheikh Ahmad, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen na kusema kuwa, Tehran inakaribisha juhudi za mjumbe huyo za kuleta mazungumzo ya kisiasa baina ya makundi ya Yemen na kuongeza kuwa, msingi mkuu wa siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuunga mkono juhudi zote za kusimamisha mara moja mashambulio ya Saudia na mapigano huko Yemen na kuanza kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo kupitia mazungumzo. Amir Abdollahiyan ameongeza kuwa, utatuzi wa mgogoro wa Yemen utapatikana tu kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa baina ya pande za Yemen kwa msaada wa pande zote za eneo hili katika kufanikisha mazungumzo hayo ya kutatua mgogoro wa Yemen. Kwa upande wake, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kadhia ya Yemen amesema kwenye mazungumzo hayo ya simu kuwa, mazungumzo ya mashauriano na Iran yanasaidia sana katika utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Yemen na pia alimueleza naibu huyo wa waziri wa mambo ya nje wa Iran kuhusu juhudi za hivi karibuni za kutatua mgogoro huo kwa njia za kisiasa. Aidha ameelezea matumaini yake kuhusu kufanikiwa juhudi za kusimamisha mapigano na kufanikisha mazungumzo pamoja na kufungua njia za kutumwa misaada ya kibinadamu huko Yemen. Hata hivyo mazungumzo hayo ya Yemen yanafanyika katika hali ambayo siku ya Jumatatu ndege vamizi wa Saudi Arabia ziliendelea kufanya mashambulizi katika maeneo tofauti ya Yemen kama vile San'a, Taiz, Ibb, Dhamar na Jawf. Makumi ya wananchi wa Yemen wakiwemo wanawake wanne na mtoto mmoja mdogo wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Katika kujibu mashambulizi hayo, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na vikosi vya wananchi limeshambulia maeneo ya mamluki wa Saudia katika mkoa wa Ibb na kuangamiza mamluki kadhaa na kuharibu zana nyingi za kivita. Aidha jeshi la Yemen na kamati za wananchi wa Yemen - licha ya kuweko mashambulizi makali ya ndege za kivita za madola vamizi - limefanikiwa kupata ushindi katika medani ya mapambano kwenye eneo la Azzabab huko Taiz na kufanikiwa kuangamiza wanamgambo 80 wa al Qaida. Wakati huo huo wnasiasa mbalimbali na watu muhimu katika masuala ya kijamii na kitaifa kwenye mkoa wa Taiz huko Yemen kwa upande wao waliitisha mkutano mkubwa na kutangaza uungaji mkono wao kwa jeshi na kamati za wananchi wa Yemen wanaoilinda nchi yao mbele ya mashambulizi ya kivamizi ya madola yanayoongozwa na Saudi Arabia.