Marekani yaunda kundi jipya la waasi Syria
Kituo cha Mapatano cha Russia nchini Syria kimetangaza kuwa, Marekani imeanzisha kundi jipya la waasi lililopewa jina la Jeshi Jipya la Syria katika kambi ya wakimbizi iliyoko mkoani Hasaka huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Ripoti zinasema, wakimbizi waliorejea makwao wanasimulia kuwa askari wa Marekani wanawapeleka wapiganaji wa kundi hilo katika maeneo ya kusini mwa Syria kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la serikali ya nchi hiyo baada ya kukamilisha mafunzo ya kijeshi.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, muungano eti wa kimataifa bado unawasiliana na wanachama waliobakia hai wa kundi la kigaidi la Daesh, na kwamba hali ya kandokando ya kambi ya wakimbizi ya Hasaka ni mfano wa wazi wa ukweli huo.
Watu walioshuhudia wamesema kuwa, muungano eti wa kimataifa unaoongozwa na Marekani dhidi ya kile kinachodaiwa ni ugaidi, kwa kipindi cha miezi sita sasa umekuwa ukitumia eneo hilo kutoa mafunzo ya kijeshi kwa waasi hao na mpaka sasa una wapiganaji 750 ambao 400 miongoni mwao ni wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh walioondolewa katika eneo la Raqqah mwezi oktoba kwa mswaada wa Marekani.
Muungano huo ulianzishwa wakati wa utawala wa Barack Obama nchini Marekani kwa kisingizio cha kupambana na magaidi katika nchi za Iraq na Syria. Hata hivyo ripoti rasmi zinasema Marekani na washirika wake wa Kimagharibi na Kiarabu wamekuwa wakishirikiana na magaidi hao hususan kundi la Daesh dhidi ya serikali ya Rais Bashar Assad nchini Syria.