Jan 09, 2018 08:18 UTC
  • Wanawafalme na viongozi 60 wa Saudia, wahamishiwa jela ya al-Ha'ir

Gazeti la Al-Araby Al-Jadeed limeandika kwamba, kwa akali wanawafalme na viongozi 60 wa ngazi ya juu wa zamani serikali nchini Saudia ambao walitiwa mbaroni na Mwanamfalme Mohammad bin Salman bin Abdulaziz Al Saud katika hoteli ya kifahari ya Ritz-Carlton ya mjini Riyadh, wamehamishiwa jela ya al-Ha'ir nchini humo.

Gazeti hilo linalochapishwa mjini London, Uingereza limewanukuu maafisa wa ngazi ya juu serikalini nchini Saudia wakisema kuwa, kati ya wanawafalme ambao wanaendelea kushikiliwa ni pamoja na Al-Waleed bin Talal na Turky bin Abdullah bin Abdulaziz Al Saud kiongozi mkuu wa zamani wa mji wa Riyadh pamoja na viongozi wa zamani wa serikali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanawafalme hao wanaendelea kushikiliwa katika korokoro za utawala huo baada ya kukataa amri ya kuigawia serikali ya Saudia fedha zao.

Mfalme Salman akiwa na mwanaye Mohammad Bin Salman wakifurahia jambo

Kwa mujibu wa gazeti la Al-Araby Al-Jadeed, bilionea Al-Waleed bin Talal amekataa katakata kumgawia Mohammad bin Salman utajiri wake na ametaka ashitakiwe kimataifa kwa kuhudhuriwa na washirika wake suala ambalo weledi wa mambo wamelitaja kuwa limemuweka Mohammad bin Salman katika mashinikizo. Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumamosi iliyopita, wanamfalme wengine 11 walitiwa mbaroni na kupelekwa jela ya al-Ha'ir baada ya kufanya maandamano mbele ya kasri la Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wakilalamikia hatua ya serikali kuwakatia ruzuku ya malipo ya maji, umeme na marupurupu mengine.

Wanawafalme wa Saudia ambao hatima yao iko mikononi mwa Mohammad bin Salman

Wakati huo huo, mtandao wa habari wa al-Ahd wa nchini Lebanon umefichua habari ya kujiri mapigano ya silaha kati ya wanawafalme watatu na walinzi saba wa jela ya al-Ha'ir ambayo yamepelekea wanawafalme hao kuuawa kusini mwa mji wa Riyadh. Tangu alipochukua hatamu za uongozi Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Waziri wa Ulinzi wa Saudia, amekuwa akitekeleza siasa za kuwashusha hadhi wanawafalme wengine ili kwa njia hiyo aweze kuvunja kambi ya upinzani dhidi yake.

Tags