Sisitizo la Umoja wa Mataifa la kutiwa mbaroni Benjamin Netanyahu
(last modified Tue, 14 Jan 2025 10:28:43 GMT )
Jan 14, 2025 10:28 UTC
  • Sisitizo la Umoja wa Mataifa la kutiwa mbaroni Benjamin Netanyahu

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Francesca Albanese ametoa wito wa kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, iwapo atazuru Poland, na kusema kuwa Warsaw lazima ifuate kanuni za haki za kimataifa.

Francesca Albanese amebainisha kuwa wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wanatakiwa kuwakamata watu ambao mahakama hiyo imetoa hati za kukamatwa kwao, na kuongeza kuwa: "Poland, ambayo ililaani kushindwa Mongolia kumkamata Rais wa Russia, Vladimir Putin, inapaswa kumkamata Netanyahu, kwa sababu ubaguzi katika utekelezaji wa sheria unadhoofisha mfumo wa haki wa kimataifa."

Mwito huo umetolewa katika hali ambayo, wananchi wa Poland walifanya maandamano katika mji wa Warsaw wakipinga uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kumpa kinga Netanyahu na kuzuia kukamatwa kwake.

Novemba 21, 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake The Hague huko Uholanzi ilitoa kibali cha kutiwa nguvuni Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wake wa vita, Yoav Gallant kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Hati ya kutiwa mbaroni Netanyahu na mshirika wake wa zamani Gallant ilitolewa baada ya kupita miezi sita tangu Karim Khan Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuwasilisha ombi la kutolewa waranti huo.

 

Hukumu hiyo ambayo haijawahi kushuhudiwa iliibua hisia kali na hasira kutoka kwa utawala wa Kizayuni hasa kwa vile kabla ya hapo utawala huu ulikuwa ukijaribu kila mara kuyafanya makundi ya muqawama ya Palestina hususan Hamas yaonekane kuwa ni magaidi na wahalifu kwa uungaji mkono wa Marekani na kujionyesha kuwa ni mhanga wao.

Hata hivyo jinai zisizo na kifani na zilizoenea na zisizofichika za Israel dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza na mauaji ya kimbari ya kukusudia, pamoja na utumiaji wa silaha ya njaa, sambamba na kuzuia kupelekwa misaada na hata kupiga marufuku shughuli za UNRWA, ni mambo ambayo yaliibua wimbi kubwa la malalamiko ya kimataifa. Mbali na hatua hizo za Israel kulaaniwa kila kona ya dunia, walimwengu walitoa wito wa kufunguliwa mashtaka maafisa wakuu wa utawala wa Kizayuni na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Nchi 124 ni wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na nchi 29 zimetia saini mkataba husika wa kimataifa wa Roma Statute, lakini hazijaidhinisha katika sheria zao za ndani.

Uamuzi huu umekabiliwa na radiamali tata na zinazopingana katika nchi za Magharibi. Mataifa ya Ulaya ambayo kimsingi karibu yote ni wanachama wa mahakama hii, sasa yanakabiliwa na mtihani mkubwa.

Hata hivyo, misimamo ya nchi hizi ni ishara nyingine ya utendaji wa kindunmakuwili wa Wazungu katika suala hili. Nchi zote za Ulaya ni wanachama wa Mkataba wa Roma na zimekubali mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Hata hivyo, nchi za Ulaya zimetoa maoni tofauti iwapo ziko tayari kutekeleza uamuzi huo au la.

Joseph Borrell, mkuu wa zamani wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, alisisitiza katika ujumbe kwenye mtandao wa X muda mfupi baada ya tangazo la Mahakama ya ICC kwamba uamuzi huu ni wa lazima na lazima utekelezwe.

Pamoja na hayo, nchi za Ulaya zimechukua misimamo tofauti katika suala hili. Ingawa Hungary ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya, mara tu baada ya uamuzi huo kutolewa, ilitangaza kwamba sio tu kwamba haitatekeleza uamuzi huu, lakini pia itamwalika Netanyahu kusafiri hadi Budapest.

Baadhi ya nchi nyingine kama vile Italia, Ireland, Ubelgiji, Uholanzi na Norway zimetangaza kwamba, zitaheshimu uamuzi wa mahakama na kwamba, zitamkamata Netanyahu ikiwa atasafiri katika nchi zao.

Baadhi ya nchi zingine hazijasema kwa uwazi kwamba zitatekeleza uamuzi huo au la. Ujerumani, kama mwanachama muhimu wa Umoja wa Ulaya, na Uingereza ziko katika kundi la nchi hizi.  Ukweli wa mambo ni kuwa, Berlin na London zitakataa kutekeleza uamuzi huu.

Licha ya kuwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Poland imesisitiza kwamba, haitamkamata Netanyahu iwapo atazuru nchi hiyo, msimamo ambao ni kinyume na ahadi zake.

Haya yanajiri licha ya kwamba Warsaw iliwahi kuikosoa Mongolia kwa kutomtia mbaroni Rais Vladimir Putin wa Russia wakati wa ziara yake nchini humo kutokana na kutolewa hati ya kukamatwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

Msimamo huu wa kindumakuwili kwa mara nyingine tena unaonyesha utendaji nchi za Magharibi katika kuchukua misimamo ya nyuso mbili kuhusiana na  masuala kama vile ugaidi, haki za binadamu na jinai za kivita.