Qatar: Iran ingelitaka ingeliweza kututesa kwa njaa
(last modified Thu, 11 Jan 2018 16:26:42 GMT )
Jan 11, 2018 16:26 UTC
  • Qatar: Iran ingelitaka ingeliweza kututesa kwa njaa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema kuwa, lau ingelitaka, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingeliweza kutumia tofauti zake za kisiasa na Doha kuwatesa kwa njaa wananchi wa Qatar, lakini kamwe haikufanya hivyo.

Mohammed bin Abdulrahman Aal Thani alisema hayo jana wakati alipohojiwa katika kipindi cha al Haqiqa cha televisheni rasmi ya Qatar na huku akigusia kuweko hitilafu za kimitazamo baina ya Iran na nchi yake katika masuala mbalimbali ya eneo hili amesema: Baada ya nchi za Kiarabu kuiwekea vikwazo vya kila namna Qatar, Iran kamwe haikutumia fursa hiyo na tofauti zake za kisiasa na Doha kutoa pigo kwa Qatar na kuwatesa kwa njaa wananchi wa nchi hiyo.

Mpaka wa Iran na Qatar

 

Vile vile amesema nchi yake iko tayari kikamilifu kutafuta njia za kutatua tofauti zake na Misri licha ya ukwamishaji mambo unaofanywa na baadhi ya pande hususan Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati). Amesema, tangu yalipotokea mapinduzi ya tarehe 25 Januari 2011 hadi hivi sasa, Misri imepitia kipindi nyeti sana lakini pamoja na hayo umuhimu wa nchi hiyo katika ulimwengu wa Kiarabu ni mkubwa, na Doha haiwezi kuingilia maamuzi ya wananchi wa Misri.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ameongeza kuwa, baada ya kupinduliwa Mohammad Morsi, rais wa zamani wa Misri mwaka 2013, kulizuka mivutano baina ya nchi yake na Misri na ingawa kumechukuliwa hatua mbalimbali lakini zimeshindwa kutatua mzozo uliopo na uhusiano wa nchi hizo mbili umeendelea kuwa baridi.

Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Juni 2017, Saudia iliongoza nchi nyingine za Kiarabu za Misri, Imarati na Bahrain kuiwekea vikwazo vya angani, baharini na ardhini nchi ndogo ya Qatar na kukata kabisa uhusiano wao na Doha. Baada ya pigo hilo, hakukuwa na nchi yoyote ambayo ingeliweza kuikoa Qatar isipokuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo nayo ilifanya uungwana wa kuwapokea mikono miwili ndugu zake wa Qatar na kufumbia macho hitilafu zote za kisiasa zilizopo baina ya nchi mbili.

Tags