UN: 75% ya wananchi wa Yemen wanahitajia misaada
Umoja wa Mataifa umesema idadi ya raia wa Yemen wanaohitajia misaada imeongezeka na kufikia milioni 22.2, huku makali ya njaa yakiongeza masaibu ya Wayemen wanaokabiliwa na mashambulizi ya Saudi Arabia kwa miaka mitatu sasa.
Katika ripoti yake iliyotolewa leo Jumanne, Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema Wayemen milioni 8 na laki nne wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa.
Ripoti hiyo imesema asilimia 76 ya wananchi milioni 29 wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu wanaishi kwa kutegemea misaada mbali mbali, hiyo ikiwa ni ongezeko la watu milioni 1.5 katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Naibu Katibu Mkuu wa UN, Mark Lowcock amesema hali ya watu wa Yemen inatia wasiwasi na ametoa wito wa kusitishwa mashambulizi ya anga yanayofanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo na kukomeshwa mapigano.
Tarehe 23 Machi mwaka 2015 Saudi Arabia na washirika wake wakisaidiwa na Marekani walianzisha mashambulizi makali ya pande zote dhidi ya Yemen kwa kile kilichotajwa kuwa ni kutaka kumrejesha madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdrabbuh Mansur Hadi aliyejiuzulu na kukimbilia Saudia.
Hadi sasa maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen wameuawa katika mashambulizi hayo na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.