Mufti wa Syria asisitiza kuhusu umoja wa nchi za Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i40511-mufti_wa_syria_asisitiza_kuhusu_umoja_wa_nchi_za_kiislamu
Mufti Mkuu wa Syria Sheikh Ahmad Badruddin Hassoun amesisitiza kuhusu ulazima wa kuungana mataifa na nchi za Kiislamu duniani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 18, 2018 03:13 UTC
  • Mufti wa Syria asisitiza kuhusu umoja wa nchi za Kiislamu

Mufti Mkuu wa Syria Sheikh Ahmad Badruddin Hassoun amesisitiza kuhusu ulazima wa kuungana mataifa na nchi za Kiislamu duniani.

Sheikh Hasoun ameyasema hayo Jumamosi katika Kikao cha Jumuiya ya Umoja wa Kiislamu Iraq mjini Baghadad na kuongeza kuwa: "Baada ya ushindi wa Baghdad katika kukabiliana na fitina ya ISIS (Daesh) na ushindi wa Syria katika kukabiliana na njama za kuigawa vipande vipande nchi, sasa umewadia wakati wa kuwepo umoja baina ya mataifa ya Kiislamu."

Mufti wa Syria amesisitiza kuhusu umoja wa Wakristo na Waislamu katika kukabiliana na uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa eti Quds Tukufu (Jerusalem) ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha amesema lengo la kuibua migogoro mingi katika eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati ni kuyafanya mataifa ya eneo hili yasahau kadhia ya Palestina na Quds Tukufu.

Mufti wa Syria pia ameituhumu Marekani kuwa inalenga kuibua vita vipya vya kidini duniani na kwa msingi huo ametoa wito kwa Wakristo duniani hasa kiongozi wa kanisa katoliki na Vatican kuchukua hatua za kukabiliana na uamuzi wa hivi karibuni wa Marekani dhidi ya Quds Tukufu.

Sehemu ya mji wa Quds

Itakumbukwa kuwa, licha ya upinzani mkubwa kieneo na kimataifa, tarehe 6 Desemba mwaka 2017, Rais wa Marekani alitangaza kuwa: Marekani inaitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa Israel.

Mji wa Quds ni mahali ulipo msikiti mtukufu wa Al Aqsa ambao ni kibla cha mwanzo cha Waislamu na ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Palestina na ni moja ya maeneo matatu makuu matakatifu ya Kiislamu yenye hadhi na umuhimu maalumu mbele ya Waislamu. Mji huo ulivamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967.