Mar 24, 2018 07:19 UTC
  • Vikosi vya Syria vyadhibiti asilimia 90 ya eneo la Ghouta Mashariki

Wanajeshi wa Syria wanadhibiti zaidi ya asilimi 90 ya eneo la Ghouta Mashariki lililo karibu na mji mkuu Damascus.

Kwa muda mrefu eneo hilo lilikuwa linadhibitiwa na magaidi wakufurishaji ambao baada ya kupata pigo sasa wanaondoka eneo hilo. Taarifa zinasema magaidi wametimuliwa kikamilifu katika mji wa Harasta ulio katika eneo hilo la Ghouta.

Leo asubuhi pia magaidi na wanamgambo wakiwa na familia zao wanatazamiwa kuondoka katika miji ya Arbin, Jobar, Zamalka na Ein Terma baada ya kufikia mapatano na serikali.

Kukombolewa eneo la Ghouta Mashariki kunatathminiwa kuwa na umuhimu mkubwa sawa na tukio la Jeshi la Syria kuukomboa mji wa Aleppo mwaka 2016.

Rais Assad wa Syria akiwa alipotembelea wanajeshi katika mstari wa mbele vitani eneo la Ghouta hivi karibuni

Eneo la kistratijia la Ghouta Mashariki limekuwa likitumiwa na magaidi kuvurumisha makombora katika mji mkuu wa Syria Damascus.

Tokea mwaka 2011, Syria imekuwa ikikabiliana na makundi ya magaidi wakufurishaji na wanamgambo wanaopata himaya ya kigeni, hasa Marekani na Saudi Arabia. Katika miezi ya hivi karibuni, Jeshi la Syria, likipata msaada wa waitifaki wake, limefanikiwa kutoa pigo kubwa kwa magaidi nchini humo.

 

Tags