Apr 11, 2018 04:33 UTC
  • Kulaaniwa wimbi jipya la kamatakamata nchini Bahrain

Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain kimetoa taarifa maalumu inayoeleza juu ya kutiwa mbaroni na vikosi vya usalama vya utawala wa Aa Khalifa wapinzani 21 na kulaani vikali hatua hiyo.

Taarifa ya kituo hicho cha haki za binadamu imelaani pia kukandamizwa maandamano 24 ya malalamiko katika maeneo 14 ya nchi hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Utawala wa Bahrain wa Aal Khalifa ukiwa na lengo la kuuzima moto wa malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo umewatia mbaroni wapinzani na wanaharakati wengi wa kisiasa wa nchi hiyo. Utawala wa Manama umewanyima wafungwa wa kisiasa hata haki ya kutembelewa na ndugu zao hatua ambayo inakinzana waziwazi na sheria za kimataifa na ni ithbati tosha kwamba, utawala huo kandamizi umeendelea kukanyanga haki za awali kabisa za wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo.

Ripoti mbalimbali kutoka Bahrain zinaonyesha kuwa, ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa kifamilia wa nchi hiyo ambao unajumuisha kutiwa mbaroni kidhulma wapinzani, kuvamiwa kiholela nyumba zao, kesi zao kuendeshwa bila ya uadilifu, kukandamizwa malalamiko na maandamano ya amani na kupokonywa uraia kumeshadidi mno.

Polisi ya Bahrain imeendelea kukandamiza maandamano ya wananchi

Utawala wa Bahrain umewanyima raia wa nchi hiyo haki zao zote za kimsingi kama uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, kufanya mikusanyiko ya amani na kuanzisha vyama na makundi ya kisiasa. Utawala huo umekuwa ukitumia kila wenzo ili sambamba na kuzima harakati ya wananchi na kuwafuta wapinzani katika ulingo wa kisiasa na kijamii, utekeleze pia siasa za kuwapokonya uraia. Wapinzani wa Bahrain wamekuwa wakipokonywa uraia sambamba na kupatiwa uraia wa nchi hiyo raia wa kigeni, uamuzi ambao una malengo ya kisiasa ambapo lengo hasa ni kubadilisha muundo wa kijamii wa nchi hiyo. 

Hatua ya utawala wa kifalme wa Bahrain ya kuwanyima raia wa nchi hiyo haki ya kuishi katika nchi hiyo nayo inakinzana wazi na haki za binadamu. Ibrahim Sahran, mshauri wa masuala ya sheria wa Bahrain anasema: idara za mahakama za Bahrain zimeharibika na kwa sasa zinatumiwa kama wenzo wa kukandamiza uhuru. Hivi karibuni wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu walitangaza katika ripoti yao kwamba: Kutokana na udhaifu na ulegevu wa mashinikizo ya jamii ya kimataifa dhidi ya Bahrain, hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo imekuwa mbaya mno katika miezi ya hivi karibuni. Brian Dooley wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights First la Marekani anasema: Hivi sasa Bahrain imo katika mkondo hatari mno.

Maandamano ya wananchi ya kupinga utawala wa Bahrain

Kwa hakika ripoti tofauti zinaonyesha kuwa, mwenendo na muamala wa kipolisi wa utawala wa Manama kwa wanaharakati wa kisiasa wa Bahrain ungali unaendelea ambapo hatua ya utawala huo ya kushadidisha kamatakamata ya wanaharakati wa kisiasa kivitendo imekuwa ikitoa mbinyo wa kisiasa dhidi ya wapinzani wa utawala huo. Ukweli wa mambo ni kuwa, moja ya matatizo makuu na ya kimsingi ya wananchi wa Bahrain na utawala wa Aal Khalifa ni muundo wa kisiasa wa nchi hiyo ambao umejengeka juu ya misingi ya udikteta na ukandamizaji.

Kuhodhiwa madaraka na utajiri na familia moja tu na watawala hao kuwawekea mipaka raia ni moja ya sababu zilizopelekea kufikia tamati subira ya wananchi wa nchi hiyo. Hali hiyo ndio iliyowafanya wananchi wa Bahrain Februari 14 mwaka 2011 waanzishe harakati ya mapinduzi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa. Hata hivyo ukandamizaji mkali wa utawala huo dhidi ya raia ndio ambao umezifanya fikra za waliowengi ulimwenguni na makundi ya kutetea haki za binadamu kuwa na wasiwasi mkubwa.

Tags