UN yatiwa wasi wasi na hali ya wanaharakati wanawake wanaozuiliwa Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i45134-un_yatiwa_wasi_wasi_na_hali_ya_wanaharakati_wanawake_wanaozuiliwa_saudia
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza juu ya wasi wasi mkubwa ilionao kuhusu hali ya wanaharakati wanawake wanaozuiliwa chini ya mazingira ya kutisha nchini Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2018 09:23 UTC
  • UN yatiwa wasi wasi na hali ya wanaharakati wanawake wanaozuiliwa Saudia

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza juu ya wasi wasi mkubwa ilionao kuhusu hali ya wanaharakati wanawake wanaozuiliwa chini ya mazingira ya kutisha nchini Saudi Arabia.

Liz Throssell, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema leo Jumanne katika mkutano mjini Geneva kuwa, sharti utawala wa Riyadh uweke bayana maelezo kuhusu hali ya wanawake hao unaowazuilia, ikiwemo haki ya kuwa na mawakili, kufahamishwa sababu za wao kukamatwa, mashitaka yanayowakabili, haki ya kutembelewa na jamaa zao na haki ya kupandishwa kizimbani ndani ya muda ulioanishwa na sheria.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Saudia yalisema Ijumaa iliyopita kwamba, vyombo vya usalama Riyadh vimeshadidisha kamatakamata dhidi ya wanaharakati wanawake, na kufikia sasa wanawake 11 wametiwa mbaroni.

Siku chache zilizopita, mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yaliutaka utawala wa Aal-Saud uwaachie huru wanaharakati hao wa kike walioongoza kampeni za kutaka kuruhusiwa wanawake kuendesha magari nchini Saudi Arabia.

Mmoja wa wanaharakati wanawake akiendesha gari nchini Saudia

Septemba mwaka jana, na baada ya harakati na malalamiko ya muda mrefu, hatimaye Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal-Saud wa Saudi Arabia alitoa amri ya kuwapa leseni za kuendesha magari wanawake wa nchi hiyo.

Hata hivyo ruhusa hiyo ya wanawake kuendesha magari nchini Saudi Arabia itaanza kutekelezwa tarehe 24 mwezi ujao wa Juni.