UN: Saudia inakandamiza na kuwatesa wanaharakati na washukiwa wa ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i45540-un_saudia_inakandamiza_na_kuwatesa_wanaharakati_na_washukiwa_wa_ugaidi
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeukosoa utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia kwa kuwakandamiza, kuwatesa na kuwadhalilisha wanaharakati na washukiwa wa ugaidi unaowazuilia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2018 10:55 UTC
  • UN: Saudia inakandamiza na kuwatesa wanaharakati na washukiwa wa ugaidi

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeukosoa utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia kwa kuwakandamiza, kuwatesa na kuwadhalilisha wanaharakati na washukiwa wa ugaidi unaowazuilia.

Haya yamebainishwa na Ben Emmerson, Ripota Maalumu wa UN anayeshughulikia masuala ya vita dhidi ya ugaidi, baada ya kutamatisha safari ya siku tano nchini Saudia.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, maafisa usalama wa Saudia wanatumia mbinu mbalimbali za ukandamizaji na utesaji dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya kigaidi nchini humo, mbali na kulazimishwa kukiri makosa ambayo hawajafanya.

Kadhalika ripoti hiyo ya UN imesema vyombo vya usalama vinawakandamiza wanaharakati wanaojaribu kutumia uhuru wao wa kujieleza, kwa kuwaweka korokoroni kwa miaka kadhaa bila kuwapandisha kizimbani.

Wanaharakati wanawake 11 wametiwa mbaroni Saudia kufikia sasa

Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema vyombo vya dola nchini Saudia vimemnyima kibali cha kutembelea magereza mbalimbali, na hata kumkataza kuonana na wanaharakati mashuhuri wa nchi hiyo.

Ben Emmerson amebainisha kuwa: Katika hali ambayo Saudia chini ya Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa nchi hiyo imeanza kuwapa wanawake leseni za kuendesha magari kwa upande mmoja, lakini pia inawatia mbaroni wanaharakati waliofanikisha kampeni hizo za kuruhusiwa wanawake kuendesha magari nchini humo, kwa upande wa pili.

Ruhusa hiyo ya wanawake kuendesha magari nchini Saudi Arabia itaanza kutekelezwa tarehe 24 mwezi huu wa Juni, lakini vyombo vya usalama Riyadh vimeshadidisha kamatakamata dhidi ya wanaharakati wanawake walioongoza kampeni za kulalamikia marufuku ya wao kuendesha magari.