Mpango wa amani wa UN nchini Yemen wataka kujumuishwa Ansarullah serikalini
Inaarifiwa kuwa, Umoja wa Mataifa umeandaa mpango wa amani wa kutamatisha mashambulizi ya muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen, baada ya jitihada za kidiplomasia kugonga mwamba.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, rasimu ya mpango huo imetayarishwa na Martin Griffiths, mjumbe wa UN nchini Yemen, ambapo ameutaka muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudia kusitisha hujuma zake dhidi ya Yemen, sambamba na kujumuishwa harakati ya Ansarullah katika serikali ijayo ya mpito.
Rasimu hiyo imesema kuwa: Silaha nyepesi na nzito yakiwemo makombora ya balestiki zinapaswa kukabidhiwa kwa mpangilio na utaratibu maalumu, na kuundwe serikali jumuishi ya mpito, ambapo mirengo na vyama vyote vya siasa vitajumuishwa.
Hata hivyo rasimu hiyo ya mpango wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen wa Umoja wa Mataifa haijaweka bayana ni kiasi gani cha uwakilishi kitatengwa kwa ajili ya Ansarullah.
Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi makali ya kikatili dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen mwezi Machi 2015 kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Imarati na kwa kutumia silaha wanazopewa na nchi za Magharibi.
Hadi hivi sasa makumi ya maelfu ya watu wameshauawa na kujeruhiwa huku Yemen ikikumbwa pia na janga la umaskini, ukame na miripuko ya magonjwa mbalimbali hatari ya kuambukiza.