Hizbullah: Tuko imara zaidi hivi sasa kukabiliana na chokochoko zozote zile
Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo ya Kiislamu iko imara zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote na kuongeza kuwa, sasa hivi Lebanon ina usalama wa kiwango cha juu zaidi katika eneo hili kutokana na ushujaa na kujitoa muhanga wanamapambano wa Kiislamu katika kukabiliana na Israel na magenge ya wakufurishaji.
Shirika la habari la RASA limemnukuu Sheikh Ali Da'amush akisema hayo na kusisitiza kuwa, kusimama imara wanamuqawama wa Lebanon mbele ya wavamizi wa Israel na kutekeleza kwao vizuri majukumu yao ya kidini na kitaifa katika kulinda nchi yao kumeiokoa Lebanon na kuilinda isiwe koloni la Wazayuni.
Amesema, daima Hizbullah ya Lebanon imekuwa ikishambuliwa na maadui kiusalama, kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kipropaganda na lengo la mashambulizi yote hayo ni kutaka kupunguza ushawishi na nguvu za Hizbullah, lakini njama zote hizo zimeshindwa kwa silaha za jihadi na subira.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hizbullah ameongeza kuwa, kitu ambacho kimevuruga njozi na tamaa zote za Israel hivi sasa ni ushirikiano madhubuti ulioko Lebanon ambao ni ushirikiano baina ya Jeshi, Wananchi na Muqawama. Amesema, siri ya mafanikio ya Lebanon ni uwezo wa kijeshi na uimara wa Hizbullah pamoja na ushirikiano madhubuti uliopo baina ya jeshi wananchi na wanamuqawama.
Sheikh Da'amush amezungumzia pia matukio ya Yemen na kusema kuwa, lengo la muungano wa Saudia la kuongeza mashambulizi dhidi ya bandari ya al Hudaydah, ni kutaka kuwatwisha wananchi wa Yemen amani wanayoitaka wavamizi wa nchi yao, lakini taifa la wanamapambano la Yemen limewathibitishia walimwengu kuwa wanastahabu kuishi kwa heshima japo kwa dhiki kuliko kuishi kwa kudhalilishwa japo kwa raha.