Wazayuni wa Israel washambulia kaburi la Nabii Yuusuf, Nablos
Makumi ya Wazayuni wa Israel wameshambulia kaburi na Nabii Yusuf (as) huko mashariki mwa mji wa Nablus katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan.
Mashambulizi hayo yaliyofanyika mapema leo Alkhamisi yamejibiwa na Wapalestina waliotoka mbio kwenda kulinda eneo hilo tukufu kwa kukabiliana na walowezi wa Kizayuni waliokuwa wakisaidiwa na jeshi la Israel.
Katika mapigano hayo maghasibu wa Israel walitumia risasi na gesi ya kutoa machozi na kuwajeruhiwa raia wawili wa Palestina. Makumi ya Wapalestina wanasumbuliwa na athari za mabomu ya gesi yaliyotumiwa na askari wa Israel katika mapigano hayo.
Katika upande mwingine mamia ya walowezi wa Kizayuni pia wameendelea kuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa kwa kuvamia eneo hilo takatifu ambalo ni kibla cha kwanza cha Waislamu wote duniani. Walowezi hao walikuwa wakitoa maneno machafu na nara zinazovunjia heshima Uislamu.
Msikiti wa al Aqsa umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na askari na walowezi wa Israel wakitaka kuharibu muundo na utambulisho wa Kiislamu wa eneo hilo na kuweka nembo za Kiyahudi mahala pale.