Sep 22, 2018 07:28 UTC
  • Udharura wa kulazimishwa Israel kujiunga na mkataba wa nyuklia wa NPT

Katika Mkutano Mkuu la 62 la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, kumesisitiziwa wajibu na udharura wa kulazimishwa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, NPT.

Mkutano Mkuu wa 62 wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ulianza Jumatatu tarehe 17 Septemba 2018 mjini Vienna, Austria na kumalizika jana Ijumaa tarehe 21 Septemba. Moja ya ajenda kuu za mkutano huo ni Mashariki ya Kati isiyo na silaha za nyuklia. Ukweli wa mambo ni kuwa, ajenda ya Mashariki ya Kati isiyo na silaha za nyuklia ndio maudhui kikuu inayojadiliwa mara zote katika Mkutano Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

Kiwanda kichakavu cha nyuklia cha Dimona cha utawala wa Kizayuni wa Israel ambacho ni hatari sana kwa usalama wa dunia nzima

 

Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia NPT ni mkataba ambao lengo lake hasa ni kuzuia uzalishaji na uenezaji wa silaha za nyuklia na kupanua wigo wa ushirikiano kwa ajili ya kutumia vizuri nishati ya nyuklia kwa njia za amani na kwa malengo ya kiraia. Mkataba huo uliundwa mwaka 1968 na ukaanza kutekelezwa rasmi mwaka 1970. Licha ya kwamba taarifa za uhakika zinasema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya nyuklia, lakini hadi leo hii unaendelea kukaidi kujiunga na mkataba huo. Amma suala lililopewa umuhimu mkubwa zaidi katika Mkutano Mkuu wa 62 wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ni kusisitiziwa udharura wa kulazimishwa utawala wa Kizayuni ujiunge na mkataba wa NPT. 

Khaled Toukan, mkuu wa taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Jordan amesisitiza katika mkutano huo juu ya wajibu wa Israel kujiunga na NPT na kusema kuwa, inabidi taasisi zote za utawala wa Kizayuni wa Israel ziwekwe chini ya uangalizi wa IAEA kwa ajili ya kulifanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa bila ya silaha za nyuklia na pia kuweza kuleta usalama na amani katika dunia nzima. 

Wakati hata Marekani na Russia zimepunguza viwanda vyao vya nyuklia, utawala wa Kizayuni wa Israel si tu kwamba bado unaendelea kufanya ukaidi wa kukataa kujiunga na NPT, lakini pia ndio kwanza unazidi kuongeza viwanda vyake vya silaha za maangamizi ya umati za nyuklia. Katika ripoti yake ya hivi karibuni, taasisi ya utafiti wa amani ya Stockholm nchini Sweden imesema kuwa, wakati ambapo Marekani na Russia zimepunguza viwanda vyao vya nyuklia, Israel ndio kwanza inazidi kuongeza na kuimarisha viwanda hivyo. 

Khaled Toukan

 

Wachambuzi wa mambo na viongozi wa kisiasa wa nchi za Mashariki ya Kati na hata wa nchi nyingine duniani wanaamini kuwa, moja ya sababu kuu za kuweko ushindani wa silaha na kuongezeka machafuko na ukosefu wa amani Mashariki ya Kati ni kukaidi utawala wa Kizayuni wa Israel kujiunga na mkataba wa NPT.

Kazem Gharib Abadi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashirika ya kimataifa yaliyoko Vienna Austria amesema katika Mkutano Mkuu wa 62 wa IAEA kwamba, njia bora ya kuweza kulinda amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati ni kuendelea kuuwekea mashinikizo mtawalia utawala wa Kizayuni wa Israel ili ujiunge na NPT. 

Ukweli wa mambo ni kuwa, matakwa ya siku zote ya nchi za Mashariki ya Kati ni kulazimishwa utawala wa Kizayuni wa Israel kujiunga na mkataba wa nyuklia wa NPT na jambo hilo halisisitizwi na nchi chache tu, bali hata nchi kama Misri ambayo ina uhusiano rasmi na Israel inatangaza wazi msimamo wake wa kutaka utawala wa Kizayuni ulazimishwe kujiunga na NPT. Viongozi wa Misri wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba kuna udharura wa kuchukuliwa hatua kali za kuilazimisha Israel ijiunge na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Atomiki, NPT.

Tags