Sep 28, 2018 07:44 UTC
  • Sheikh mmoja mkubwa afariki dunia akiwa jela nchini Saudi Arabia

Vyombo vya habari nchini Saudia vimetangaza habari ya kufariki dunia Safar al-Hawali, mmoja wa wanazuioni wakubwa wa nchi hiyo akiwa katika jela za utawala wa Aal Saud.

Tangu mwanachuoni huyo alipotiwa mbaroni na maafisa usalama wa Saudia alikuwa mgonjwa, huku serikali ikikataa kumpa matibabu sambamba na kupuuza hali yake mbaya ya kimwili. Al-Hawali, alitiwa mbaroni mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu baada ya kutoa kitabu alichokipa jina la 'Waislamu na Utamaduni wa Magharibi' ambacho ndani yake msomi huyo alisema kuwa, hatua ya kuipatia kiasi kikubwa cha fedha serikali ya Marekani na kadhalika kumpatia mabilioni ya Dola, Donald Trump wakati wa safari yake nchini Saudi Arabia haina faida yoyote.

Mohammad Bin Salman ambaye anatumia mkono wa chuma ili aweze kutawala Saudia

Hayo yanajiri katika hali ambayo tarehe 14 Agosti mwaka huu wapinzani wa serikali ya Saudia walifichua habari ya kufariki dunia Suleiman Al-Dawash, mmoja wa viongozi wa kidini wa nchi hiyo akiwa katika jela kutokana na mateso aliyoyapata kutoka kwa maafisa usalama. Hadi sasa makumi ya wafanyabiashara, viongozi wa kidini, wanawafalme, maulamaa, malenga, wahadhiri wa vyuo vikuu na wanaharakati wa kiraia hususan wanawake, wametiwa mbaroni tangu alipoteuliwa Mohammad Bin Salman kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia.

Tags