Hamas: Baadhi ya nchi za Kiarabu zinaichochea Israel iishambulie Gaza
Mwanachama wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ametahadharisha kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu zinaushawishi utawala wa Kizayuni utekeleze mashambulizi huko Ghaza.
Mahmoud al Zahar amesisitiza kuwa baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu na Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wanaandaa mipango ili pamoja na kuishinikiza Hamas ibadilishane mateka, Israel iweze kutekeleza mashambulizi katika Ukanda wa Ghaza. Al Zahar hakutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo wa nchi za Kiarabu hata hivyo amesema kuwa baadhi ya hatua za Mahmoud Abbas kama kusitisha kuhamishia fedha katika mabenki ya Ghaza zinatekelezwa kwa lengo la kuwafanya wakazi wa eneo hilo kuwa dhidi ya Hamas.
Mamlaka ya Ndani ya Palstina imekata asilimia 50 ya mishahara ya wafanyakazi wa Ghaza ili kuiweka chini ya mashinikizo harakati ya Hamas. Si hilo tu, mamlaka hiyo imepunguza pia mgao wa umeme na utumaji wa misaada ya kitiba katika eneo hilo. Hatua hizo za Mamlaka ya Ndani ya Palestina chini ya uongozi wa Mahmoud Abbas zimewapelekea maelfu ya Wapalestina kustaafu kwa lazima huku ulipaji wa mishahara yao na wafanyakazi wengine ikiwa imesimamishwa kwa miezi kadhaa sasa.