Oct 06, 2018 07:16 UTC
  • HRW: Saudia iweke na uwazi kuhusu mwandishi habari Jamal Khashoggi

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka Saudi Arabia iwe na sera za wazi kuhusu mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa nchi hiyo Jamal Khashoggi aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuingia katika ubalozi wa Saudi Arabia nchini Uturuki.

Taarifa iliyotolewa na Human Rights Watch imesema kuwa, kutoweka kwa mwandishi habari na mkosoaji wa siasa za serikali ya Saudi Arabia, Jamal Khashoggi ambaye mara ya mwisho alikuwa katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, ni mgogoro mwingine wa haki za binadamu kwa serikali ya Riyadh.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Kama Saudi Arabia imemficha Khashoggi, hatua hiyo itatambuliwa kuwa ni utekaji nyara, na Riyadh inapaswa kuthibitisha kwamba mkosaji huyo alitoka nje ya ubalozi wake mjini Istanbul. Mwandishi na mkosoaji huyo mkubwa wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia alitekwa nyara tarehe pili mwezi huu wa Oktoba akiwa ndani ya ubalozi wa  Saudia mjini Istanbul, Uturuki.

Jamal Khashoggi

Jina la Jamal Khashoggi lilikuwa katika orodha ya watu wanaosakwa kwa udi na uvumba na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na kwa msingi huo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema kuwa ametekwa nyara kwa amri ya Bin Salman. 

Serikali ya Uturuki imemsaili balozi wa Saudia mjini Istanbul kuhusiana na kadhia ya kutoweka mwandishi huyo mashuhuri. Mkosoaji maarufu Msaudi, Mujtahidi ambaye ni mashuhuri kwa kufichua habari za ndani ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo ameandika kuwa, Jamal Khashoggi ametekwa nyara na kwa sasa anashikiliwa nchini Saudi Arabia.  

Tags