Maelfu ya Wapakistan wanashikiliwa katika jela za Saudia na Imarati
Waziri wa zamani wa Masuala ya Ustawi wa Kieneo katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa nchini Pakistan amefichua kwamba, jumla ya raia 3,309 wa nchi hiyo wanashikiliwa katika jela za Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa Inayatullah Khan, aghlabu ya raia hao wa Pakistan wanabughudhiwa na kunyanyaswa na wasimamizi wa jela za utawala wa Saudia. Amesisitiza kwamba kutokana na miamla mibaya ya wasimamizi wa jela, baadhi ya wafungwa wamechukua hatua ya kujiua. Kufuatia taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Makhdoom Shah Qureshi sambamba na kuthibitisha habari hiyo ya kuendelea kushikiliwa zaidi ya raia elfu tatu wa nchi hiyo katika jela za Saudia, amesema kuwa raia wengine wa Pakistan wapatao 2,600 wanashikiliwa katika jela za Imarati.
Hayo yanajiri katika hali ambayo asasi za kutetea haki za binaadamu zimetangaza kwamba, aghlabu ya raia wa nchi za kigeni walioenda Saudia kwa ajili ya kutafuta ajira, wamekuwa wakifanyishwa kazi ngumu sambamba na kukabiliwa na matatizo mengi ikiwemo wafanyakazi wanawake kubakwa na waajiri wao, kunyimwa mishahara, kunyanyaswa kimwili sambamba na kutishiwa kutimuliwa pale wanapolalamika. Licha ya Pakistan kulalamikia mwenendo huo mbaya wa serikali ya Riyadh kwa raia wake, lakini misaada ya kifedha ambayo inapewa serikali ya Islamabad na Saudia, imeifanya nchi hiyo ifumbie macho haki za kimsingi za raia wake. Hivi karibuni pia Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia ilitoa taarifa ikisema kuwa, tokea mwaka 2011 hadi sasa utawala wa Saudia, umewahukumu kifo raia 103 wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, raia hao wa Indonesia ambao kimsingi ni wafanyakazi wa kazi za ndani ya nyumba, tayari wamekwishanyongwa au wanasubiri kunyongwa.