Yemen katika ukingo wa shimo la maafa makubwa ya kibinadamu
Mark Lowcock, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya misaada ya kibinadamu amesema kuwa, misaada zaidi inahitajika kwa ajili ya wananchi wa Yemen katika mwaka ujao wa 2019 na kutahadharisha kuwa, nchi ya Yemen iliyoharibiwa vibaya na vita iko katika ukingo wa shimo la maafa makubwa ya kibinadamu.
Kwa upande wake, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni alisema kuwa ,Yemen ndio mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu na kwamba sasa hivi nchi hiyo iko kwenye ncha kabisa ya kutumbukia katika shimo la maangamizi.

Hatua ya viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa ya kutahadharisha kuhusu hali mbaya ya Yemen pamoja na takwimu kubwa kubwa zinazotolewa kuhusu maafa ya kibinadamu nchini humo kiasi kwamba viongozi hao wa Umoja wa Mataifa wameongeza mashinikizo yao ya kutaka kukomeshwa mara moja mgogoro huo, ni ushahidi wa hali mbaya sana waliyo nayo wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu na inabidi jamii ya kimataifa iichukulie kwa uzito wa hali ya juu kabisa hali hiyo. Jukumu la kukomesha maafa ya kibinadamu huko Yemen ni wajibu wa kihistoria wa dunia nzima leo hii. Muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kwa kutumia silaha angamizi unazopewa na madola ya kibeberu ya Magharibi hasa Marekani, unafanya jinai za kuchupa mipaka kwa miaka minne sasa tena mbele ya macho ya jamii ya kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ulimwenguni. Muungano huo vamizi umewabebesha wananchi wa Yemen maafa yasiyo na kifani kama mauaji, ukimbizi, magonjwa na ukame na hivi sasa nchi hiyo ya Kiislamu imekuwa kituo kikuu cha mgogoro wa kibinadamu duniani.
Hata hivyo muungano huo vamizi umeshindwa kupata mafanikio yoyote ghairi ya kuharibu miundombinu yote ya Yemen na kuwasababishia wananchi maskini wa nchi hiyo mabalaa yasiyoelezeka. Saudi Arabia kwa kushirikiana na genge lake ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati, inashambulia misikiti, maskuli, mahospitali, viwanja vya ndege, madaraja, nyumba za raia, viwanda, taasisi za serikali na kila kitu ambacho kinawanufaisha raia wa kawaida. Wavamizi hao makatili hawahurumii hata mabasi ya watoto wa madrasa na skuli, bali wanashambulia kiholela kila wanachokiona mbele yao.

Amma cha kusikitisha zaidi ni kuwa, licha ya kutendeka jinai zote hizo, lakini Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema Jumamosi ya juzi pambizoni mwa kikao cha kundi la G20 katika mji mkuu wa Brazil, Buenos Aires kwamba, nchi yake itaendelea na ratiba zake kama kawaida za kuisheheneza silaha Saudi Arabia licha ya kwamba anakiri kuwa hali ya kibinadamu nchini Yemen ni mbaya sana. Hii ni katika hali ambayo, siku ya Jumatano iliyopita, kamati ya uhusiano wa kigeni ya baraza la Sanate la Marekani ilipasisha kwa wingi wa kura uamuzi wa kusimamishwa misaada ya kijeshi ya Marekani kwa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen. Maseneta 63 waliunga mkono mpango wa kusimamishwa misaada hiyo dhidi ya 37 waliopinga. Wakati huo huo taasisi ya kuwaokoa watoto wadogo yenye makao yake nchini Uingereza imesema kuwa, karibu watoto 85 elfu wa Yemen wenye chini ya umri wa miaka 5 wameshapoteza maisha yao kutokana na lishe duni tangu Saudia ilipoivamia nchi hiyo ya Kiarabu mwaka 2015.
Kwa upande wake, Rand Paul, seneta wa chama cha Republican cha rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa, Saudi Arabia ndiyo inayobeba dhima ya mauaji ya makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen kwa msaada wa Marekani. Seneta huyo ameitaka Marekani kuangalia upya misaada na uhusiano wake kwa Saudi Arabia. Hivi karibuni pia kanali ya televisheni ya Aljazeera ya Qatar imetangaza kuwa, Marekani ndiye mbeba dhima ya janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani walilobebeshwa wananchi wa Yemen. Taasisi tano za misaada ya kibinadamu zinazoendesha shughuli zake nchini Yemen nazo zimetoa taarifa ya pamoja na kuitahadharisha Marekani kutokana na nafasi yake kubwa mbaya katika maafa ya kibinadamu waliyo nayo wananchi wa Yemen hivi sasa.
Kwa kweli uungaji mkono wa pande zote wa Marekani kwa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia huko Yemen ndiyo sababu kuu ya kuendelea kushuhudiwa masaibu ya wananchi hao Waislamu kwa mikono ya koo za Aal Saud, Aal Nahyan na watenda jinai wenzao wengine.