Sababu za kuvunjwa bunge la Israel
Wabunge wa bunge la Israel (Knesset) wamepasisha muswada wa kulivunja bunge hilo na kuitisha uchaguzi wa kabla ya wakati wake katika ardhi hizo za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Uchaguzi wa bunge la Israel umepangwa kufanyika mwezi Aprili 2019, miezi saba kabla ya wakati wake. Swali kuu linalojitokeza hapa ni kwamba, ni nini hasa sababu ya kusambaratika Baraza la Mawaziri la serikali ya mseto ya utawala wa Kizayuni na ni jambo gani limepelekea kuchukuliwa uamuzi wa kuitishwa uchaguzi wa bunge kabla ya wakati wake?
Kimsingi kuna sababu aina mbili yaani za ndani na za nje ya utawala wa Kizayuni ndizo zilizopelekea kutumbukia utawala huo pandikizi katika mkwamo huo.
Sababu za nje ndizo ambazo zimechangia sana kusambaratika serikali ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Sababu ya kwanza kabisa ni hatua ya Netanyahu ya kukubali mpango wa kusimamisha vita katika Ukanda wa Ghaza. Mwezi Oktoba mwaka huu, jeshi la Israel liliuvamia Ukanda wa Ghaza na kuua kigaidi makamanda kadhaa wa muqaawama, lakini uvamizi huo ulipata majibu makali sana kutoka kwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS. Utawala wa Kizayuni ulilazimika kusimamisha uvamizi wake huo siku mbili tu tangu baada ya kuivamia Ghaza kutokana na kujibiwa kwa makombora na maroketi 460 kutoka kwa wanamapambano wa Palestina. Vita hivyo vya siku mbili viliifedhehesha vibaya "Ngao ya Chuma" ya Israel ya kujilinda na makombora kwani haikutungua isipokuwa maroketi na makombora 100 tu kati ya hayo 460 ambapo yaliyobakia yote yalipiga kulikokusudiwa. Pigo la kwanza kabisa lililosababishwa na fedheha hiyo ni kujiuzulu Evigdor Lieberman, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni na hivyo kuinyima serikali ya Netanyahu wingi wa viti bungeni. Baada ya hapo, chama cha kidini cha HaBayit HaYehudi yaani Nyumbani kwa Mayahudi kinachoongozwa na Naftali Bennett nacho kilijitoa katika serikali na huo ukawa msumari wa mwisho juu ya jeneza la serikali ya Benjamin Netanyahu.
Tukija upande wa ndani wa utawala wa Kizayuni tutaona kuwa, mizozo mingi ndani ya serikali ya mseto ya Benjamin Netanyahu pamoja na mivutano chungu nzima baina ya serikali hiyo na bunge, ni miongoni mwa sababu kuu ya kusambaratika serikali ya Netanyahu na kuchukuliwa uamuzi wa kuitishwa uchaguzi wa bunge miezi saba kabla ya wakati wake.
Kikao cha siku ya Jumatatu baina ya viongozi wa serikali ya Isrel na bunge la utawala huo wa Kizayuni kilishindwa kufikia makubaliano ya kuzuia kusambaratika serikali ya Netanyahu. Moja ya sababu zilizopelekea kufeli kikao hicho ni mzozo kuhusu kupasishwa sheria ya kibaguzi inayojulikana kwa jina la "Serikali - Taifa la Kiyahudi."
Benjamin Netanyahu alitetea kwa nguvu zake zote sheria hiyo ya kibaguzi akisema: Sheria hiyo inaonesha uaminifu wetu kwa Israel kwani sheria tunazoopitisha zinaonesha uaminifu wa kila mmoja wetu kwa wakazi wa Israel.
Hata hivyo baadhi ya vyama vinavyounda serikali ya mseto ya utawala wa Kizayuni vinaipinga sheria hiyo. Kiujumla ni kwamba kukataa bunge la Israel kupasisha muswada uliopendekezwa na serikai ya Benjamin Netanyahu wa kutumiwa Mayahudi wenye misimamo mikali katika mambo mbalimbali ni moja ya sababu za ndani ya utawala wa Kizayuni iliyopelekea kusambaratika serikali na kuchukuliwa uamuzi wa kuitishwa uchaguzi wa bunge wa kabla ya wakati wake.
Tzipi Livni, mmoja wa viongozi wanaoipinga serikali ya Netanyahu amesema: Sisi hatumtaki tu Netanyahu, ni sawa sheria hiyo iwepo au isiwepo. Netanyahu lazima aondoke. Hakuna usalama wala demokrasia yoyote Israel na gharama za maisha nazo zimepanda sana.
Sababu nyingine ya ndani ya utawala wa Kizayuni iliyopelekea kusambaratika serikali na kuitishwa uchaguzi wa bunge wa kabla ya wakati wake ni maandamano na malamiko makubwa ya wakazi wa Israel kutokana na hali mbaya ya maisha.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, dalili zote zinaonesha kwamba uwaziri mkuu wa Benjamin Netanyahu umemalizika na hata ikitokezea kushinda chama chake ciha Likud katika uchaguzi wa bunge wa mwezi Aprili 2019, si rahisi kwa chama hicho kumchagua yeye tena kuwa waziri mkuu.