Washington Post: Mohammad bin Salman amezidisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani
Gazeti la Washington Post la Marekani limeanika kwamba Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia na mtuhumiwa nambari moja wa mauaji dhidi ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa Saudia, anaendelea kufanya ukandamizaji dhidi ya wapinzani wake nchini humo.
Katika makala iliyopewa jina la 'Mashine ya ukandamizaji inayosonga mbele kwa mwendo wa kasi' Washington Post limeandika kwamba, si tu kwamba Bin Salman hajabadilisha mienendo yake ya ukandamizaji, bali anaendeleza kampeni yake ya ukatili dhidi ya wapinzani kwa kutumia mbinu za utawala wa kidikteta.
Gazeti hilo la Marekani limeandika kwamba, miongoni mwa mambo yanayoonyesha kwamba Mohammad Bin Salman hajabadili mbinu za kutia khofu kupitia intaneti, ni kampeni yake ya mashambulizi iliyoanza wiki hii katikaa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii dhidi ya Jamal Khashoggi na Omar Abdul Aziz, mpinzani wa Saudia anayeishi nchini Canada.
Khashoggi aliuawa tarehe pili Oktoba mwaka jana kwa amri ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia nchini Uturuki. Hata hivyo serikali ya Marekani sambamba na kumtetea Bin Salman na kumkingia kifua, imeendelea kunyamanzia kimya jinai hiyo.