Wimbi jipya la mauaji ya Israel dhidi ya watoto wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50921-wimbi_jipya_la_mauaji_ya_israel_dhidi_ya_watoto_wa_palestina
Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu cha Mizan kimetangaza kuwa, watoto 50 wa Kipalestina waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mwaka uliomalizika majuzi wa 2018 na wengine elfu 2 na 890 wamejeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2019 23:14 UTC
  • Wimbi jipya la mauaji ya Israel dhidi ya watoto wa Palestina

Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu cha Mizan kimetangaza kuwa, watoto 50 wa Kipalestina waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mwaka uliomalizika majuzi wa 2018 na wengine elfu 2 na 890 wamejeruhiwa.

Ripoti ya kituo hicho imesema kuwa: Israel inaendelea kukanyaga haki za Wapalestina hususan watoto wadogo na mwaka jana ilishambulia kwa mabomu na kubomoa shule 2 katika Ukanda wa Gaza.

Kuanzia mwaka 2000 wakati ilipoanza harakati ya Intifadha ya Pili, karibu watoto elfu 2 na 300 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika mashambulizi ya askari wa utawala haramu wa Israel. Sasa na kwa mara nyingine ripoti za jumuiya mbalimbali za haki za binadamu zimemulika tena mienendo ya utawala huo katili ambao umekuwa maarufu kama utawala unaoua watoto. La kusikitisha zaidi ni kuwa, utawala huo unaua watoto wadogo ambao si tishio kwa askari wa Israel. Mienendo hiyo na askari wa Israel imekemewa na kulaaniwa na jumuiya nyingi za kutetea haki za binadamu. Mwandishi habari wa Marekani, Richard Silverstein ameitaja Israel kuwa ni utawala unaoua watoto. Silverstein anasema: Israel imefanya dhulma kubwa na nyingi dhidi ya watoto wa Palestina na inawalenga na kuwashambulia moja kwa moja. Israel inaua watoto wa Kipalestina ambao hawakufanya kosa lolote.

Mwaka 2018 Israel imeua watoto hamsini wa Kipalestina.

Israel inaendelea kufanya ukatili wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuua watoto wa Palestina kutokana na kimya cha jumuiya za kimataifa, na idadi kubwa ya watoto waliouawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala huo katika mwaka uliopita wa 2018 ni ushahidi wa wazi wa ukweli huo. Baya zaidi ni kuwa, viongozi wa utawala huo haramu wamekuwa wakisisitiza na kutoa wito wa kuuliwa watoto wa Kipalestina. Katika kikao cha baraza la mawaziri la utawala huo kilichofanyika mwaka jana, Waziri wa Elimu wa Israel, Naftali Bennett alitoa wito wa kushambuliwa moja kwa moja watoto wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wanaotuma maputo ya baruti katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Bennett alisema watoto hao wanapaswa kushambuliwa kwa kutumia ndege za kivita au ndege zisizo na rubani. 

Utawala haramu wa Israel unaongoza kati ya tawala zinazokiuka sheria za kimataifa kwa kuwakamata watoto, kuwahukumu na kuwapa mateso ya aina kwa aina katika jela za kutisha za utawala huo.

Mauaji ya raia wa Palestina yanayofanywa na utawala haramu wa Israel sasa yamekuwa jambo la kawaida na sehemu ya utamaduni wa viongozi wa utawala huo kwa kadiri kwamba, hakuna siku inayopita bila ya kuripotiwa habari ya ukatili na mauaji ya askari hao dhidi ya Wapalestina hususan watoto na mabarobaro. Jinai, ukatili na mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto wa Palestina ni kinyume na sheria za kimataifa hususan kifungu nambari 16 cha makubaliano ya kimataifa ya haki za watoto. Kifungu hicho kinapiga marufuku mienendo yoyote ya kikatili dhidi ya watoto.

Watoto wa Kipalestina waliouawa na askari wa Israel, Gaza.

Vilevile mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wakiwemo watoto ni kielelezo halisi cha jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari. Haya yote yanafanyika huku Umoja wa Mataifa ukiendelea kushikwa na kigugumizi mbele ya mauaji na jinai hizo za utawala katili wa Israel. Umoja huo na taasisi zake kama Baraza Kuu la Haki za Binadamu zimekataa hata kuiweka Israel katika orodha ya nchi zinazokiuka haki za watoto duniani. Misimamo kama hii ndiyo inayozidisha kiburi cha Israel na kuushajiisha utawala huo haramu kuendelea kuua watoto wadogo wa Palestina bila ya woga wala wasiwasi wa kusailiwa na yeyote.