UN yakosoa fichaficha ya Saudi Arabia kuhusu mauaji ya Khashoggi
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia visa vya kunyongwa watu kiholela na kinyume cha sheria amewatuhumu viongozi wa Saudi Arabia kuwa wanakwamisha uchunguzi wa faili la kesi ya mauaji ya mwandishi habari mkosoaji wa utawala huo, Jamal Khashoggi.
Bi Agnes Callamard amesema kuwa, viongozi wa Saudi Arabia walikwamisha jitihada za Uturuki za kuchunguza mahali alipouliwa Jamal Khashoggi mwandishi habari aliyekuwa akiukosoa utawala wa Saudi Arabia.
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa licha ya kuwasilishwa maombi mara kadhaa lakini hadi kufikia sasa viongozi wa Saudi Arabia na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA)) hawajatoa ushirikiano wowote na maafisa wa UN.
Jamal Khashoggi aliuawa tarehe Pili Oktoba mwaka jana ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki. Mashirika ya ujasusi likiwemo shirika la ujasusi la Marekani CIA yamethibitisha kuwa mauaji hayo yalitekelezwa kwa amri ya Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ambaye anakingiwa kifua na Rais Donald Trump wa Marekani.