Jeshi la Yemen laangamiza mamluki 90 wa Saudia vitani
Jeshi la Yemen limetangaza kuwaangamiza mamluki 90 wa Saudi Arabia katika mji wa Sa'ada wakati wa kuzima hujuma kubwa ya Wasaudi dhidi ya mji huo wa kaskazini-magharibi mwa Yemen.
Msemaji wa Jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesema wanajeshi wa Yemen walizima hujuma iliyokuwa inaongozwa na Saudia katika Wilaya ya Baqim ambapo mamluki 90 waliangamizwa na wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa.
Amesema Jeshi la Yemen limewatimua kikamilifu mamluki wa Saudia kutoka katika miinuko ya Naseh. Siku ya Jumapili Saree alisema wanajeshi wa Yemen walikuwa wamewaua wanajeshi 20 wa Saudia kama njia ya kulipiza kisasi kutokana na hujuma ya Saudia dhidi ya nchi hiyo. Vita vya Saudia dhidi ya Yemen vimeingia mwaka wa tano mwezi huu wa Machi.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi.
Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia wasiopungua 15,000 ambao wamepoteza maisha moja kwa moja vitani. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel. Vita hivyo vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen aidha vimepelekea karibu Wayemen milioni 3 kuwa wakimbizi na kati ya watu milioni 24 nchini Yemen, takribani milioni 22 wanahitaji msaada wa chakula.