Ngao ya anga ya Syria yatungua makombora ya Israel
Syria imetangaza kuwa, mfumo wa ulinzi wa anga wa jeshi la nchi hiyo umefanikiwa kutungua makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel karibu na mji wa Hama.
Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kuwa, ndege ya kivita ya utawala haramu wa Israel imefanya mashambulio ya makombora katika mji wa Masyaf, mkoani Hama, katikati mwa nchi.
Habari zaidi zinasema kuwa, miripuko mikubwa imesikika katika sehemu mbalimbali ya mkoa huo, na kwamba watu watatu wamejeruhiwa, huku majengo kadhaa yakiharibiwa.
Kwa mujibu wa SANA, shambulizi hilo la anga la utawala wa khabithi wa Israel lililolenga kambi ya kijeshi karibu na mji wa Hama limefanywa kwa kutumia anga ya Lebanon.
Mara kwa mara utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya mashambulizi ya kivamizi ndani ya ardhi ya Syria ili kuyalinda magenge ya kigaidi na ya ukufurishaji kama vile Daesh (ISIS) na Jabhat al Nusra.
Hata hivyo aghalabu ya mashambulio hayo huzimwa na mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya anga wa Syria wenye uwezo wa kutungua makombora yote ya adui kabla ya kufika yaliyokokusudiwa.
Syria imekumbwa na mgogoro tangu mwaka 2011 baada ya magaidi kumiminika nchini humo kutokea kila upande kwa msaada wa Saudi Arabia, Marekani, Israel na waitifaki wao, lengo kuu likiwa ni kujaribu kulinda usalama wa utawala wa Kizayuni unaokikalia kwa mabavu Kibla cha Kwanza cha Waislamu.