Saudi Arabia inatumia adhabu ya kifo kuangamiza upinzani
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amesty International linasema Saudi Arabia inatumia adhabu ya kifo kuwaangamiza wapinzani huku mrithi wa kiti cha ufalme Mohammad bin Salman akiendeleza ukandamizaji dhidi ya wahubiri wa Kiislamu, wanahabari na wasomi katika ufalme huo.
Amnesty International imesema mwendesha mashtaka mkuu Saudi Arabia amependekeza wapinzani zaidi wapewe adhabu ya kifo huku ikibainika kuwa mhubiri mashuhuru Sheikh Salman al-Awdah ni miongoni mwa wale ambao yamkini watahukumiwa kifo.
Watetezi wa haki za binadamu wanasema Sheikh al-Awdah na wahubiri wengine wawili ambao ni Awad al-Qarni and Ali al-Omari wamekuwa gerezani kwa muda wa miezi 19 kinyume cha sheria.

Aidha mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake Saudia Bi. Khadijah al-Harbi, ambaye yuko katika siku za mwisho za ujauzito, alikamatwa wiki iliyopita huku utawala wa kiimla wa Saudia ukiendelea kuzihadaa nchi za Magharibi kuwa eti unawawezesha wanawake.
Katika kipindi cha takribani miaka miwili sasa, hususan baada ya kuteuliwa Muhammad bin Salman kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ambaye anafuata siasa za Marekani na Israel, makumi ya wafanyabiashara, wanazuoni, wanawafalme na maulamaa wa nchi hiyo wametiwa mbaroni na kufungwa jela kwa kupinga sera zake.